WAKULIMA wa kahawa wanaohudumiwa na Chama kikuu cha Ushirika wilaya ya Mbinga (MBIFACU),katika kipindi cha miaka mitatu wamefanikiwa kuongeza uzalishaji wa zao hilo kutoka tani 12,000 msimu wa kilimo 2020/ 2021 hadi tani 20,000 katika msimu wa kilimo 2023/2024.
Kaimu Meneja wa MBIFACU Faraja Komba amesema, ongezeko la uzalishaji limetokana na mikakati ya Serikali ya awamu ya sita ya kuwainua wakulima.
Amesema,mpango wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutoa pembejeo za ruzuku kwa wakulima umehamasisha na kuwavutia watu wengi kujikita kwenye kilimo cha zao la kahawa.
Komba amesema,katika kipindi cha miaka mitatu wakulima wameongeza takribani tani 8 sawa na kilo milioni 8 ambazo ni mafanikio makubwa katika sekta ya ushirika na wakulima wa kahawa kwa ujumla.
Amesema,kuanzia mwaka 2021 hadi 2024 wametoa mikopo ya mbolea yenye thamani ya Sh.bilioni 11 kwa wakulima wanaojihusisha na kilimo cha kahawa na serikali imeunga mkono kwa kutoa Sh.bilioni 10.6. zilizokwenda kwa wakulima kupitia vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS).
Komba ameishukuru serikali kuboresha masoko ya kahawa,kwani sasa wakulima wanatumia masoko matatu(soko la awali,soko la mnadani na soko la mauzo ya moja ambayo yamesaidia kurahisisha mauzo ya kahawa na wakulima kupata fedha zao kwa wakati.
Hata hivyo, ameiomba serikali kupitia wizara ya kilimo na ushirika kuwaangalia kwa jicho la huruma wakulima wa kahawa kwa kuendelea kuwapa mikopo na pembejeo za ruzuku ili waweze kuendelea kuzalisha kahawa kwa wingi.
Amesema,serikali ikiendelea kutoa pembejeo hasa mbolea za ruzuku,uzalishaji wa kahawa katika wilaya ya Mbinga utaongezeka kutoka tani 20,000 na kufikia malengo ya kuzalisha tani 35,000 ifikapo mwaka 2030.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.