Wakulima wa zao la kahawa katika Kijiji cha Kingerikiti, Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kusimamia kwa mafanikio bei ya zao hilo katika soko la dunia, kutoka Sh. 3,000 mwaka 2021/2022 hadi Sh. 8,500 kwa kilo moja. Wamesema ongezeko hilo limeleta mafanikio makubwa katika maisha yao na kuchochea ari ya kuendelea na kilimo hicho.
Mkulima Vitus Mapunda amesema awali walikumbwa na changamoto ya bei ndogo ya kahawa huku gharama za uzalishaji zikiwa juu, hali iliyowafanya kuishi maisha magumu licha ya juhudi kubwa mashambani. Hata hivyo, amepongeza Serikali kwa kuboresha hali hiyo kupitia sera madhubuti za kilimo, hasa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Mapunda ameongeza kuwa upatikanaji wa mbolea za ruzuku umechangia ongezeko la uzalishaji kutoka tani nne hadi kufikia tani kumi kwa ekari moja. Hii imetokana na usimamizi mzuri wa Serikali katika kila hatua ya uzalishaji wa kahawa, kuanzia maandalizi ya shamba hadi kuuza mazao sokoni.
Hata hivyo, Mapunda na wakulima wengine wameitaka Serikali kuongeza maafisa ugani katika kila kijiji badala ya kuishia ngazi ya kata, ili wakulima wengi waweze kufikiwa na kuelimishwa kuhusu kilimo bora. Wamesema ukosefu wa elimu hiyo unarudisha nyuma jitihada za kuongeza uzalishaji wa mazao mashambani.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Msingi cha Ushirika wa Kilimo na Masoko Kingerikiti, Fabian Ndunguru, amesema kupitia ushirikiano wa kimataifa, Amcos yao imepata ufadhili kutoka Marekani wa Sh. milioni 588, fedha zitakazotumika kujenga miundombinu muhimu kama maabara ya kahawa, sehemu ya kukaanga na ghala la kuhifadhi mazao. Hii ni hatua kubwa kuelekea kuongeza thamani ya zao hilo na kuongeza kipato cha wakulima.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.