WAKULIMA wa ufuta wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,wamezidi kuvuna fedha kufuatia bei ya zao hilo kupanda kutoka Sh.3,022 kwa kilo moja katika mnada wa pili hadi Sh.3,095 katika mnada wa tatu uliofanyika katika Chama cha msingi cha Ushirika Mluji(Amcos) kijiji cha Mchesi.
Meneja masoko wa Chama kikuu cha Ushirika wilayani Tunduru(Tamcu Ltd) Marcelino Mrope alisema,katika mnada wa tatu jumla ya kilo 670,040 zenye thamani ya Sh.bilioni 2,073,773.800 zimekusanywa na kuuzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani na wakulima wanaohudumiwa na Chama chama hicho.
Aidha alisema, katika mnada wa kwanza jumla ya kilo,1,008,638 zenye thamani ya Sh.bilioni 3,008,700.143 ziliuzwa kwa wastani wa bei ya Sh.2,982.93 na katika mnada wa pili kilo 507,522 zenye thamani ya Sh.bilioni 1,533,916,440.00 ziliuzwa kwa bei ya Sh.3,022 kwa kilo moja.
Alisema,katika minada miwili ya awali jumla ya ufuta uliouzwa ni kilo 1,516,160 zenye thamani ya Sh.bilioni 4.5 kati ya fedha hizo bilioni 4.4 zimekwenda kwa wakulima pamoja na watoa huduma ambao ni wasafirishaji.
Akifunga mnada huo Mwenyekiti wa Tamcu Mussa Manjaule alisema, jumla ya makampuni tisa yalijitokeza katika mnada huo,lakini ni makampuni matatu tu ya Export Trading,Yuri Investment na Rv Export yaliyokubaliwa kununua ufuta katika mnada wa tatu.
Manjaule,amewapongeza wakulima kwa kukubali kuuza ufuta wao kwa bei nzuri na kuwataka kuongeza kasi ya uzalishaji katika msimu ujao.
“wakulima wa wilaya ya Tunduru wanaishukuru sana serikali kwa kufanya maamuzi ya kuwakomboa wakulima wake kwa kuuza mazao yao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umeendelea kuwa na manufaa makubwa kwa wakulima”alisema.
Alisema,serikali imefanya maamuzi sahihi kuanzisha minada ya ufuta na baadhi ya mazao na hayo ni mfanikio na ukombozi mkubwa wa kiuchumi kwa wakulima wa wilaya ya Tunduru.
Manjaule,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kutoa pembejeo kwa wakulima wa korosho bure,hata hivyo amewakumbusha wakulima kujiwekea akiba ya fedha wanazopata kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa zao la korosho, badala ya kuzitumia fedha hizo kwenye mambo yasiofaa ikiwamo ulevi.
Manjaule ambaye ni mjumbe wa bodi ya KoroshoTanzania,amewakumbusha wakulima kulipa madeni yote wanayodaiwa na taasisi za fedha ili wawe na sifa ya kukopesheka kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za kilimo.
Amewataka kufungua akaunti kwa ajili ya kuingiziwa malipo yao,badala ya kutumia akaunti za watu wengine ambao baadhi sio waaminifu ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.
Kwa upande wake Afisa Ushirika wa wilaya ya Tunduru George Bisani alisema, katika msimu wa mwaka huu uzalishaji wa zao la ufuta sio mkubwa kutokana na wakulima wengi kujikita sana kwenye zao la Alizeti na mbaazi.
Bisani,amewaomba wakulima wa Tarafa ya Lukumbule kuongeza ukubwa wa mashamba yao na kulima mazao mchanganyiko ili kujiongezea kipato, badala ya kujikita kwenye zao moja tu la Korosho au Ufuta.
Amewaasa,kuendelea na utaratibu wa kuuza ufuta na mazao mengine kwa mfumo wa stakabadhi ghalani,kwani tangu ulipoanzishwa umekuwa na manufaa makubwa si kwa wakulima wenyewe bali hata kwa wafanyabiashara na Serikali kwa ujumla.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima wengine Yusufu Twaha,ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuimarisha mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umewasaidia sana wakulima kuwa na uhakika wa soko na kupata bei nzuri.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.