Wananchi wa Mamlaka ya mji mdogo wa Namtumbo Mkoani Ruvuma wameiomba serikali mradi wa uchimbaji wa madini ya Urani katika Kijiji cha Likuyu.
Wananchi hao wametoa ombi hilo kwenye mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Mheshimiwa Vitta Kawawa wa kusikiliza kero za wananchi uliofanyika Kata ya Rwinga mjini Namtumbo.
Wananchi hao walisema mradi wa uchimbaji wa madini ya Urani katika Kijiji cha Likuyu umebaki kimya kwa muda mrefu licha ya kupewa matumaini ya kuanza Kwa mradi huo.
Shami Kingovaye mwananchi wa kata ya Rwinga ametoa rai kwa serikali kuanza kutekeleza mradi huo ambao amesema utachangia maendeleo ya wilaya ya Namtumbo na Taifa kwa ujumla.
Kingovaye amesema wananchi wa Namtumbo wana matumaini makubwa ya kuanza Kwa mradi huo ambao utawanufaisha wananchi kiuchumi Kwa kuuza bidhaa zao kupitia mkusanyiko wa watu watakaokuwepo wakati wa uchimbaji wa madini hayo.
Rashid John Mkazi wa Likuyu amesema wananchi wa Namtumbo hasa vijana wanatarajia kupata ajira mbalimbali kutokana na kuanza Kwa mradi huo .
Mbunge wa Namtumbo Vitta Kawawa pamoja na kuwashukuru wananchi wa kata ya Rwinga kutumia muda wao na kuhudhuria mkutano wake Ili waweze kuelezea kero zao.
Akijibu kero ya kuchelewa kuchimba madini ya Urani Mheshimiwa Kawawa alisema Kuna changamoto iliyojitokeza kati ya TANAPA na kampuni iliyopewa jukumu la kuchimba madini hayo hali iliyochelewesha mradi huo kuanza kutekelezwa.
Amesema Kampuni ya MANTRA iliyopewa jukumu la kuchimba madini hayo ilikumbana na kikwazo hicho na kusubiria utaratibu mwingine unaofanywa na Serikali ili mradi huo uanze kutekelezwa na wananchi kuanza kunufaika.
Hata hivyo Mheshimiwa Kawawa alibainisha kuwa awali changamoto ilikuwa eneo linalotakiwa kuchimba madini hayo lipo katika hifadhi na eneo ambalo ni urithi wa Dunia( world heritage) na kwamba kulingana na Sheria za kimataifa za uhifadhi haitakiwi kufanyika shughuli yoyote ya kibinadamu bila idhini ya Mamlaka husika kwenye eneo la urithi wa Dunia.
Hata hivyo Mbunge huyo wa Namtumbo alisema kuwa Serikali ililiondoa eneo hilo kwenye hifadhi Ili kuiwezesha Kampuni ya MANTRA iliyopewa idhini ya kuchimba madini hayo iweze kuchimba na kwamba kampuni hiyo haikuweza kuanza mradi wa kuchimba madini hayo baada ya kushuka bei katika soko la Dunia.
Ameeleza kuwa wakati Kampuni hiyo inasubiri bei nzuri katika soko la Dunia, Serikali iliamua eneo hilo kulitoa kwenye hifadhi kutoka hifadhi ya Taifa ya Selous Kwa wakati ule na kukitenga kipande Cha eneo kilichokuwa na madini ya Urani na kukipa jina la Undendeule forest Ili kuruhusu madini hayo yaweze kuchimbwa Kwa manufaa makubwa ya taifa.
Amesema baada ya hifadhi kuitwa hifadhi ya Taifa ya Nyerere na kuwa chini ya TANAPA kumejitokeza changamoto tena kwa TANAPA kuhusu kutokuwa na taarifa ya uchimbaji huo wa madini katika maeneo ambayo yapo chini yao ambapo Serikali inalifanyia kazi suala hilo na kulitafutia ufumbuzi ili wananchi waanze kunufaika na mradi huo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.