Baadhi ya wananchi wa Tunduru mkoani Ruvuma,wamempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ya kusimamia na kuboresha sekta ya afya ambayo awali ilikabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uchakavu wa majengo,upungufu wa dawa,vifaa tiba na watumishi hasa katika maeneo ya vijijini.
Wameishukuru serikali kwa uamuzi wa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa zahanati, vituo vya afya na Hospitali ya wilaya Tunduru hali iliyowezesha upatikanaji wa huduma bora za matibabu wilayani humo.
Said Halfani alisema,kwa sasa wanafurahi na matumaini makubwa kuona serikali imeamua kutoa fedha ili kuboresha huduma za afya hasa katika Hospitali ya wilaya Tunduru ambayo ni tegemeo kubwa kwa watu wa wilaya hiyo kongwe hapa nchini.
Hussein Yusuf alisema,kabla ya ukarabati wa majengo na ujenzi wa majengo mapya katika Hospitali hiyo ikiwemo jengo la wagonjwa wa dharura hapo awali walilazimika kwenda Hospitali nyingine kama Hospitali ya Misheni Mbesa na Ndanda kwa ajili ya kufuata huduma za dharura ambazo zilikosekana katika Hospitali ya wilaya.
Yusuf licha ya kuipongeza serikali kwa kazi nzuri inayofanya,ameiomba kuhakikisha ukarabati huo unaendeane na utoaji wa huduma bora kwa watu wanaofika kupata matibabu.
Aidha,ameitaka serikali kuhakikisha inawachukulia hatua baadhi ya watumishi wazembe wanaofanya kazi kwa mazoea na wale wanaotoa lugha chafu kwa wagonjwa wanofika kupata huduma.
Halvina Masangano mkazi wa mtaa wa Majengo Tunduru mjini,amefurahishwa na ubora wa majengo mapya,lakini ameiomba serikali kuongeza idadi ya watumishi kwani waliopo ni wachache kutokana na Hospitali hiyo kuwa kimbilio kubwa la wananchi wa wilaya ya Tunduru.
Kwa upande wake mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya Tunduru Dkt Athuman Mkonoumo alisema,kwa sasa hali ya upatikanaji wa huduma za afya katika Hospitali ya wilaya Tunduru zimeimarika baada ya serikali kutoa Sh.bilioni 1.270 kwa ajili ya kufanya ukarabati wa baadhi ya majengo ya kutolea huduma za afya.
Dkt Mkonoumo alisema,kati ya fedha hizo Sh.milioni 900 zimetumika kufanya ukarabati wa jengo la wagonjwa wa nje(OPD),Maabara na jengo la upasuaji huku Sh.milioni 370 zimefanikisha kujenga jengo jipya la wagonjwa wa dharura(EMD).
Ameishukuru serikali kuwapatia fedha kwa ajili ya ukarabati wa majengo ambayo yamesaidia kuboresha huduma hasa ikizingatiwa kumekuwa na ongezeko kubwa la wateja wanaofika kwenda kupata huduma katika Hospitali hiyo.
Alisema,ukarabati na ujenzi wa majengo hayo ikiwemo jengo la dharura umekamilika kwa asilimia 100 na majengo yote mapya yameanza kutoa huduma,hivyo kupunguza rufaa kwa baadhi ya wagonjwa kwenda nje ya wilaya ya Tunduru kufuata huduma zaidi za matibabu.
Alisema,ukarabati huo umerahisisha utendaji kazi kwa watumishi wa Hospitali kwa sababu ya kuwepo kwa vifaa na miundombinu ya kisasa tofauti na hapo awali ambapo kulikuwa na majengo machache na chakavu.
Ameipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa kufanya ukarabati mkubwa wa jengo maalum la upasuaji ambalo limekuwa msaada mkubwa kwa mama wajawazito wanaofika kujifungua kwa njia hiyo ambapo idadi yao inafikia zaidi ya 80 kwa mwezi.
Dkt Mkonoumo alisema,Hospitali ya wilaya Tunduru ni kati ya Hospitali kongwe hapa nchini na kwa muda mrefu haijawahi kufanyiwa ukarabati,kwa hiyo majengo yake mengi yalikuwa chakavu hivyo kukwamisha mkakati wa serikali wa kutoa huduma bora na za kisasa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.