Baadhi ya wanawake wamekuwa wakifanya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanaume wao, hasa wale ambao wamepata fursa za kipato.
Tabia hii inatajwa kusababisha msongo wa mawazo kwa wanaume, hali inayoweza kuchangia vifo vyao vya mapema.
Katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, wanawake wa mkoa wa Ruvuma wamehimizwa kuacha tabia hiyo.
Akizungumza katika kongamano la wanawake wa Ruvuma, Mbunge wa Viti Maalum wa mkoa huo, Mhe. Jacqueline Ngonyani Msongozi, alisema kuwa mwanamke kuwa na kipato haimaanishi kumvunjia heshima mume wake.
Alisisitiza kuwa heshima kwa mume ni wajibu wa mwanamke, hata kama anajitegemea kifedha.
Mhe. Msongozi alibainisha kuwa baadhi ya wanaume wanapitia changamoto kubwa za kisaikolojia kutokana na ukatili wa wake zao, hali inayowafanya kushindwa kufurahia maisha ya ndoa. Alisema kuwa heshima na maelewano kati ya wanandoa ni msingi wa familia imara na yenye furaha.
Aidha, aliwahimiza wanawake kutumia fursa za kiuchumi kuboresha maisha ya familia zao badala ya kuzitumia kama sababu ya kudharau au kutawala wanaume wao. Alieleza kuwa mafanikio ya mwanamke yanapaswa kuwa chachu ya maendeleo ya familia nzima, si chanzo cha migogoro.
Kuelekea Siku ya Wanawake Duniani, wanawake waliombwa kujitathmini na kuhakikisha kuwa wanachangia katika kujenga jamii yenye usawa na heshima kwa wote. Wito ulitolewa kwa wanandoa kushirikiana kwa kuheshimiana ili kuepuka athari za msongo wa mawazo unaoweza kuleta madhara makubwa kwa wanaume.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.