Wataalam wa afya mkoani Ruvuma wamepatiwa mafunzo ya Chati Uchungu iliyoboreshwa (Labour Care Guide) inayosaidia kufuatilia maendeleo ya mama mjamzito na mtoto wake tumboni kabla ya kujifungua.
Mafunzo hayo yatakayofanyika kwa siku 5 kuanzia Machi 17 hadi 21, 2025, yanajumuisha washiriki 40 kutoka Halmashauri zote 8 za Mkoa wa Ruvuma, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Songea, Hospitali ya Rufaa ya Peramiho, pamoja na wakufunzi wa vyuo vya Afya na Sayansi Shirikishi vya Peramiho, Litembo, Kiuma na Songea.
Afisa Muuguzi kutoka Wizara ya Afya, Machimu Venance, amesema Chati Uchungu iliyoboreshwa inatoa nafasi kwa mama anayejifungua hospitalini kuwa na mtu wake wa karibu kama mume, mama yake au rafiki, ili kuwa naye kwa kipindi chote cha kujifungua ambapo mpango huo unalenga kuboresha hali ya mama wakati wa kujifungua.
Kwa upande wake, Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Hilda Ndambalilo, amesema Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma imeandaa mafunzo hayo maalum yanayolenga kuboresha huduma za afya kwa kina mama wajawazito na watoto wachanga.
Amesisitiza kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana kwa sababu yanatoa uelewa wa kina juu ya ufuatiliaji wa kina mama wakiwa katika chumba cha kujifungua, ili kuhakikisha wanapata huduma bora na salama na kupunguza vifo vya wajawazito au wazazi na watoto wachanga.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.