Wazazi na walezi Wilayani Mbinga wametakiwa kuwa chachu ya mabadiliko ya kukua kwa elimu na wale wote watakaobainika kuhujumu jitihada za serikali katika kukuza sekta ya elimu kwa kuhamasisha watoto wao kufanya vibaya kwa makusudi kwenye mitihani yao wamepewa onyo kali na kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Hayo yamebainishwa wakati wa kikao cha Tathmini ya Elimu Tarafa ya Mbuji kilichofanyika Aprili 22, ambapo baadhi ya wadau waliohudhuria kikao hicho wameibua hoja na mjadala kuhusu baadhi ya wazazi na walezi kuhujumu kwa makusudi jitihada za serikali katika kuboresha elimu kwa namna mbalimbali na kupelekea watoto kufanya vibaya kwenye mitihani yao ya mwisho licha ya wanafunzi hao kuwa na uwezo mzuri darasani.
Akizungumza kwenye kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Shule ya Mtakatifu Charles Borromeo, Kijiji cha Myau kata ya Mbuji na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa elimu, Afisa Elimu Mkoa wa Ruvuma, Emmanuel Kisongo amesema suala la usimamizi na ukuaji wa sekta ya elimu ni wajibu wa kila mmoja katika jamii nzima kuanzia ngazi ya familia na kwamba ni aibu kubwa kwa mzazi kulazimisha na kusababisha mtoto wake kufeli mtihani.
Bw. Kisongo amesisitiza kuwa jukumu la usimamizi wa elimu ni la kila mmoja na kwamba changamoto nyingi zilizotolewa kwenye kikao hicho zipo ndani ya uwezo wa jamii akitolea mfano utoro, mimba kwa wanafunzi, wazazi kutochangia chakula na mahitaji muhimu huku akitoa wito kwa jamii kuacha kulalamika na kutaka kila mmoja kekemea, kuchukua hatua na kuwajibika kulingana na nafasi yake.
“Wajibu wa usimamizi wa elimu ni wetu sote, hakuna kulalamika tuchape kazi na kukemea maovu hakuna mtu wa kukomboa watoto na jamii ya mbinga zaidi ya sisi wenyewe; tukiamua tunaweza” Amesema Bw. Kisongo.
Imeelezwa kuwa baadhi ya wazazi wamekua wakiwapa vitisho watoto wao kwa kuwalazimisha kutoandika majibu sahihi kwenye mitihani, kuwatorosha watoto kipindi cha mitihani, kukwepa kutoa michango na mahitaji ya shule huku baadhi wakidaiwa kujihusisha na imani za kishirikina mashuleni na kupelekea wanafunzi kwenye shule hizo kushuka kitaaluma.
Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mwl. Samwel Komba ambaye ni Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ametoa taarifa kuwa hadi sasa jumla ya wanafunzi wanne (4) wamepata mimba, watatu kati yao wakiwa tayari wameshaandikishwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu na kukemea tabia ya baadhi ya wazazi na jamii kukwepa kutoa ushahidi na kesi nyingi kumalizwa nje ya mahakama na kuwataka kutoa ushirikiano kila wanapotakiwa kufanya hivyo.
Kikao cha Tathmini ya Elimu Tarafa ya Mbuji kimefanyika ikiwa ni mwendelezo wa vikao hivyo vinavyofanyika kwenye ngazi ya Tarafa ili kufanya tathmini ya hali ya ukuaji wa taaluma kwa kubainisha, kupitia na kujadili changamoto mbambali zinazoikabili sekta ya elimu na kuweka mikakati na maazimio ya pamoja yanayokusudia kuinua hali ya taaluma ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kwa kushirikisha wadau wa elimu kama Madiwani, Watendaji wa Kata na Vijiji, Maafisa Elimu na wataalamu wengine ngazi ya kata na vijiji, wajumbe wa bodi na Kamati za Shule na wadau wengine muhimu.
Imeandikwa na: Salum Said
Afisa Habari Mbinga
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.