WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na maboresho yaliyofanyika katika hospitali ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa Oktoba 18, 2022 alipofanya ziara hospitalini hapo.
Mheshimiwa Waziri Mkuu alipofanya ziara katika hospitali hiyo na alieleza kutorishwa na milango iliyowekwa na kuagiza iondolewe na iwekwe mingine yenye viwango na leo Januari 06, 2023 amekagua maendeleo ya utekelezaji wa agizo na ameridhishwa na kazi iliyofanyika.
Kufuatia utekelezaji huo Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na utekelezaji wa maelekezo hayo ambapo hadi sasa jumla ya milango 67 kati ya 84 imeondolewa na kuwekwa mipya yenye ubora.
“Leo nimeona milango bora kabisa, kwa nini tulikubali kuweka milango mibovu wakati mizuri ipo? Hii haikubaliki kwa sababu tunapoteza fedha za Serikali zinazotokana na kodi ya wananchi. Ni lazima kila mtumishi wa umma atimize wajibu wake.”
Amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya afya ili kusogeza huduma muhimu za kijamii karibu na wananchi.
Pia, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Idara katika halmashauri zote nchini wasimamie kikamilifu utekelezaji wa shughuli zote za maendeleo katika maeneo yao ili kuhakikisha fedha zinazoidhinishwa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa miradi zinatumika ipasavyo.
“Haipendezi kuona viongozi wakuu waje na kubaini madudu katika miradi wakati watendaji mpo. Kila mtumishi awajibike ipasavyo katika eneo lake ili kuhakikisha lengo la Mheshimiwa Rais Dkt. Samia la kuwaletea maendeleo wananchi linatimia.”
Mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 7.5, mpaka sasa hospitali hiyo imepokea shilingi bilioni 4.2 kutoka Serikali kuu ambapo majengo 20 yameshajengwa, majengo 13 yamekamilika, majengo saba yapo katika hatua za ukamilishaji. Hospitali itakapokamilika inatarajia kuhudumia watu Zaidi ya 200,000.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange amesema Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuiboresha sekta ya afya ikiwemo kununua magari mawili kwenye halmashauri zote 184 nchini ikiwa moja nila wagonjwa na linguine ni kwa ajili ya usimamizi wa huduma za afya.
Akizungumza kuhusu ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Namtumbo, Dkt. Dugange amesema watahakikisha wanasimamia maagizo yote yaliyotolewa na Waziri Mkuu ili kuhakikisha shule hiyo inakamilika kwa wakati na inaanza kudahili wanafunzi
Awali, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt. Christopher Wabarumi aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za afya katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo na wilaya hiyo ambayo inaendelea na ujenzi wa majengo ya 22 katika hospitali ya wilaya hiyo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.