Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana,Ajira na Watu wenye Ulemavu Prof.Joyce Ndalichako ameziagiza Halmashauri zote nchini kutenga bajeti ya mafuta kinga kwa ajili ya watu wenye ualbino.
Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo wakati anazungumza kwenye hotuba yake iliyosomwa na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mheshimiwa Kapenjama Ndile katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya uelewa kuhusu ualbino yaliyofanyika kitaifa kwenye uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.
“Ninafahamu mafuta kinga yameingizwa katika mnyororo wa ugavi wa manunuzi ya dawa wa MSD,ninatambua kuwa upatikanaji wa mafuta haya unaweza kuwa si toshelevu,tengeni bajeti na ofisi yangu itafanya ufuatiliaji wa karibu wakati wote kwenye vituo vya afya’’,alisisitiza Ndalichako.
Amesema Ofisi ya Waziri Mkuu katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 ilitenga bajeti ya shilingi milioni 50 kwa ajili ya kuboresha upatikanaji wa mafuta kinga kwa watu wenye ualbino nchini.
Hata hivyo amesema katika eneo la afya serikali imeendelea kuboresha huduma za afya kwa kujenga vituo vya kutolea huduma za afya vilivyo na miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu.
Amesisitiza kuwa serikali imeendelea kuyapa kipaumbele masuala ya watu wenye ulemavu ikiwa ni Pamoja na masuala ya elimu,uwezeshaji wa kiuchumi,afya,ajira,nyenzo za kujimudu na mafunzo ya ufundi stadi.
Amebainisha zaidi kuwa serikali inatambua kuwa watu wenye ualbino bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali na kwamba serikali imedhamiria kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu nchini wanapata haki zao za msingi Pamoja na ustawi wa Maisha yao ya kila siku ndani ya familia na jamii inayowazunguka.
Amesema serikali imeendelea kufufua vyuo vya ufundi stadi na kufanya marekebisho kwa ajili ya mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 serikali inaendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa vyuo vipya na marekebisho ya vyuo vya ufundi stadi katika mikoa ya Ruvuma,Songwe na Kigoma.
Ameongeza kuwa serikali imeendelea kuajiri vijana wenye ulemavu katika kada mbalimbali ambapo kuanzia mwaka 2020 hadi 2023 serikalini imeajiri watumishi wenye ulemavu 812 na kwamba katika programu ya ukuzaji ujuzi kuanzia mwaka 2021 hadi 2023 jumla ya vijana wenye ulemavu 569 wamepatiwa mafunzo.
Waziri Ndalichako pia amewaagiza maafisa Ustawi wa Jamii kuhakikisha takwimu za watu wenye ualbino zinapatikana katika maeneo yao kwa ajili ya kupata huduma muhimu.
Awali risala ya watu wenye ualbino kwenye maadhimisho hayo iliyosomwa na Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wwenye ulemavu nchini Erenest Kimaila imezitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili kuwa ni upatikanaji wa vifaa kinga vya kudhibiti saratani ya Ngozi kwa wenye ualbino ikiwemo mafuta kinga na vifaa vya upasuaji baridi (cryosurgery equipment).
Haya ni maadhimisho ya 17 kitaifa na maadhimisho ya saba kitaifa kwa watu wenye ualbino yenye kauli mbiu ujumuishi ni uimara(inclusion is strength).
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wwenye ulemavu nchini Erenest Kimaila akizungumza kwenye maadhimisho ya siku kimataifa ya siku ya uelewa kuhusu watu wenye ualbino
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.