WILAYA tano mkoani Ruvuma zinatarajia kunufaika na mradi wa umeme wa REA awamu ya tatu utakaogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 70 ifikapo Desemba mwaka huu.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na waziri wa Nishati Dkt.Medard Kalemani wakati alipokuwa akizungumza na wananchi kwenye uzinduzi wa mradi huo uliofanyika kimkoa katika kata ya Nalasi wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.
Dkt. Kalemani alizitaja wilaya zitakazonufaika na mradi huo wa umeme wa REA awamu ya tatu kuwa ni Tunduru,Namtumbo,Songea,Mbinga pamoja na wilaya ya Nyasa.
Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo waziri huyo alisema kuwa serikali ya awamu ya sita imedhamiria kufikikisha umeme huo wa REA kwenye vijiji na vitongoji vyote vilivyosalia katika wilaya hizo ndani ya miezi 18.
Aidha amewataka wananchi hao kutumia fursa hiyo ya kuingiza umeme huo kwa gharama ya shilingi 27,000 katika kuanzisha viwanda vidogo vidogo kwa lengo la kuchochea uchumi wa mtu mmoja mmoja pamoja na kuiingizia serikali mapato.
Hata hivyo waziri Kalemani ametoa maagizo na maelekezo mbalimbali kwa kandarasi zinazotekeleza mradi huo ikiwa pamoja na kuacha kuruka kijiji,kuacha kuwatoza wananchi gharama za nguzo,kuacha kubagua nyumba za kuingiza umeme na kuhakikisha Tanesco inafungua ofisi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi kwenye maeneo hayo.
Naye mkuu wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Balozi wilbart Ibuge amemshukuru na kumpongeza waziri Kalemani kwa jitihada zake za kuhakikisha wananchi wa vijiji mbalimbali mkoani humo wanafikiwa na huduma hiyo huku akitoa rai kwa jamii kuacha tabia ya kuharibu miundombinu ya umeme kwa madai kwamba yeyote atakayebainika kufanya hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM)mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho alisema kuwa chama chake kinafurahishwa kuona serikali ikiendelea kutekeleza Ilani ya chama hicho ambayo waliahidi kwa wananchi wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Tunduru kusini Daimu Mpakate amemshukuru rais Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ambapo katika kata ya Nalasi jimboni humo umeme huo unatarajiwa kuwashwa Agosti mwaka huu.
Imeandikwa na Julius Konala
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.