Katika juhudi za kuhakikisha ardhi ya Tanzania inatumiwa kwa tija zaidi, Wizara ya Kilimo kupitia Kitengo cha Matumizi Bora ya Ardhi imepewa jukumu la kupima afya ya udongo nchi nzima.
Zoezi hili linafadhiliwa na mkopo kutoka Benki ya Dunia (World Bank) na linahusisha upimaji wa hali ya afya ya udongo ili kuzalisha ramani zitakazobainisha aina za udongo, kutoa mapendekezo juu ya ardhi inayofaa kwa kilimo, mazao yanayofaa kwenye maeneo husika pamoja na aina za mbolea zinazokidhi mahitaji ya udongo huo.
Kutokana na umuhimu wa Mkoa wa Ruvuma kama mzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula, Wizara ilianza zoezi hili katika mkoa huo. Timu ya wataalamu wabobezi hamsini (50) iliundwa kutoka taasisi mbalimbali.
Taasisi hizo ni Pamoja na Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Chuo Kikuu cha Nelson Mandela, pamoja na watafiti waliopo na wastaafu wa masuala ya afya ya udongo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Mlingano Tanga na Uyole.
Pia, wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo kupitia Idara ya Matumizi Bora ya Ardhi walihusika katika utekelezaji wa zoezi hili.
Timu ya wataalamu iliwasili mkoani Ruvuma mnamo Septemba 2024 na kuanza kazi ya uchukuaji wa sampuli za udongo kwa kutumia mwongozo wa picha za satelaiti na "coordinates".
Halmashauri na vijiji vyote vya Songea Vijijini na Manispaa, Nyasa, Mbinga Mji, Mbinga Vijijini, Tunduru na Namtumbo vilihusika katika zoezi hili.
Hata hivyo, kutokana na ufinyu wa bajeti, Halmashauri ya Madaba haikuweza kushirikishwa, lakini mipango ipo kwamba sampuli za udongo kutoka eneo hilo zitakusanywa kupitia mradi mwingine utakaotekelezwa mkoani Njombe.
Baada ya sampuli kukusanywa, zilipelekwa maabara kwa ajili ya uchambuzi zaidi ili kuhakikisha zoezi la upimaji linafanikiwa. Lengo kuu ni kusaidia wakulima wa Tanzania kupata taarifa sahihi kuhusu udongo wao, hivyo kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu aina ya mazao ya kupanda na mbolea zinazofaa kwa matumizi yao.
Hii ni hatua muhimu katika kuboresha kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao kwa tija zaidi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.