Katika kijiji kidogo cha Likuyu, wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, historia mpya ya Tanzania iliandikwa mbele ya maelfu ya wananchi waliokusanyika kwa shauku kubwa kushuhudia tukio la kihistoria. Ni hapa ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alizindua rasmi kiwanda cha majaribio cha kuchenjua madini ya urani – mradi wa kwanza wa aina yake nchini Tanzania na wa kipekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Ni hatua ya kimkakati inayoliingiza Taifa kwenye ramani ya dunia kama mzalishaji na mtoaji mkubwa wa malighafi adimu ya nishati safi. Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), bara la Afrika linakadiriwa kuwa na takribani asilimia 20 ya hifadhi ya madini ya urani duniani, lakini ni nchi chache sana zinayochakata madini hayo ndani ya mipaka yao. Sasa Tanzania inajiunga rasmi na kundi hili dogo, kwa mbwembwe na matumaini makubwa.
“Tanzania itakuwa kwenye ramani ya dunia kama moja ya wachangiaji wakuu wa malighafi hii muhimu ya nishati safi,” alieleza kwa msisitizo Rais Samia, huku akishangiliwa na wananchi waliofurika viwanjani.
Mradi huu unaosimamiwa na Kampuni ya Mantra Tanzania Limited ni wa kimkakati kitaifa, ukibeba dira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na kufikia uchumi wa kati wa juu unaojitegemea. Hii siyo ndoto tu — ni hatua ya vitendo inayoambatana na uwekezaji mkubwa wa kimataifa wa takribani dola bilioni 1.2 za Kimarekani, sawa na zaidi ya shilingi trilioni 3 za Kitanzania, ndani ya kipindi cha miaka 20 ya uzalishaji.
Lakini faida za mradi huu haziishii tu kwenye uchumi wa makaratasi. Tayari inakadiriwa kuwa utazalisha ajira kati ya 3,500 hadi 4,000, zikiwemo ajira za kudumu 750 kwa vijana wa Kitanzania. Hili ni ongezeko la fursa kwa jamii husika, hasa kwa wakazi wa vijiji vya jirani wanaotarajiwa kunufaika moja kwa moja kupitia ajira zisizohitaji ujuzi maalum, kama alivyoagiza Rais Samia.
Rais Samia alibainisha kuwa ujenzi wa kiwanda hicho umezingatia viwango vya kimataifa vya usalama wa mazingira na afya ya binadamu. Serikali imejizatiti kuhakikisha kuwa pamoja na uzalishaji, usalama wa watu na mazingira umepewa kipaumbele cha juu. Hii ni pamoja na kufuata miongozo ya kitaalamu inayotolewa na mashirika ya kimataifa kama Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA).
"Tumeweka mikakati ya kuhakikisha kila hatua inatekelezwa kwa uangalifu, kwa faida ya wananchi na taifa kwa ujumla," alisisitiza Dkt. Samia.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, alisema mradi huu wa majaribio ni hatua ya mwanzo tu kuelekea ndoto kubwa zaidi—ujenzi wa mtambo mkubwa wa kuchakata madini ya urani. Akasema:
“Hakuna nchi nyingine katika Afrika Mashariki na Kati inayomiliki au kupanga kujenga mradi wa aina hii; Tanzania inachukua nafasi ya kipekee.”
Kwa miaka mingi, Ruvuma imekuwa ikijulikana kwa mazao ya kilimo kama mahindi, mpunga na kahawa. Leo, jina la mkoa huu linaanza kutajwa kwenye muktadha wa kimataifa wa nishati mbadala. Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, alieleza kwa fahari jinsi mradi huo unavyobeba matumaini makubwa ya mabadiliko ya kijamii na kiuchumi kwa mkoa huo.
“Tunaamini kuwa urani italeta mabadiliko makubwa katika sekta za elimu, afya na miundombinu. Huu ni mwanzo wa enzi mpya ya maendeleo kwa Ruvuma,” alisema Kanali Ahmed.
Kwa mujibu wa tathmini ya kiuchumi, mapato yanayotarajiwa kutoka kwenye mradi huu yanaweza kuongeza pato la Taifa kwa kiwango kikubwa, na kuchochea miradi mingine ya kimkakati ikiwa ni pamoja na barabara, shule, hospitali, maji safi, na huduma nyingine muhimu za kijamii.
Uzinduzi wa mradi wa urani Namtumbo si tu alama ya maendeleo ya kiuchumi, bali pia ni ushahidi wa uthubutu wa uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Katika dunia inayokimbilia nishati safi na endelevu, Tanzania sasa imejipambanua kama sehemu ya suluhisho. Kupitia sera madhubuti, uwekezaji thabiti, na usimamizi makini, Taifa linapiga hatua kubwa — kutoka kijiji cha Likuyu hadi majukwaa ya dunia.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.