Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, amefanya ziara ya kutembelea soko la Bombambili lililopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, kwa lengo la kusikiliza na kujibu kero mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara wa soko hilo.
Katika mkutano huo, wafanyabiashara wamewasilisha kero kadhaa ikiwemo kufungiwa vibanda vya biashara, ubovu wa barabara, uwepo wa majengo mabovu ambayo hayatumiki, vumbi linalosababisha usumbufu kwa wateja, pamoja na kuwepo kwa magenge mitaani ambayo yanadaiwa kuwazuia watu kufika sokoni kununua bidhaa.
Akijibu baadhi ya hoja hizo, Afisa Biashara wa Manispaa ya Songea, Lusajo Mwasongwe, ameeleza kuwa sababu za kufungia vibanda vya biashara ni kutokana na wafanyabiashara kutolipa kodi ya pango, huku vibanda vingine vikiwa bado havijakamilika kwa matumizi rasmi.
Baada ya kusikiliza kero hizo pamoja na majibu kutoka kwa maafisa husika, Kanali Ahmed ametoa maagizo kwa wahusika kuhakikisha changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa soko hilo zinatatuliwa kwa haraka.
Amemuagiza Afisa Biashara wa Manispaa ya Songea kutofungia vibanda vya biashara, na badala yake kuweka mpango wa kuwawezesha wafanyabiashara kulipa kodi ya pango kidogo kidogo huku wakiendelea na shughuli zao katika vibanda hivyo.
Kuhusu ubovu wa barabara, Mkuu wa Mkoa ametoa muda wa wiki mbili kwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuhakikisha barabara zinachongwa sokoni hapo ili kuboresha mazingira ya biashara.
Akizungumzia suala la magenge yaliyopo mitaani, ameelekeza kuandaliwa utaratibu utakaomuwezesha mfanyabiashara anayetoka maeneo ya mbali kununua bidhaa sokoni hapo kupata fursa ya kuuza bidhaa katika maeneo wanayotokea, hata kwa kuweka vituo maalum vya mauzo, badala ya kufunga magenge yao ili kuwawezesha wananchi kupata unafuu wa maisha kupitia biashara hizo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.