Katika kile kinachoonekana kama ukurasa mpya wa mageuzi ya kilimo nchini, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua rasmi Kiwanda cha Mbolea cha ITRACOM kilichopo eneo la Nala jijini Dodoma.
Rais ametoa rai kwa uongozi wa kiwanda hicho kuhakikisha mbolea inawafikia wakulima hadi vijijini kwa gharama nafuu.
Tukio hilo limewakutanisha viongozi mbalimbali wa kitaifa na kimataifa, akiwemo Rais wa Burundi, Meja Jenerali mstaafu Evariste Ndayishimiye.
Rais Samia alisisitiza umuhimu wa kuweka mfumo madhubuti wa usambazaji wa mbolea hiyo ya FOMI ili kila mkulima, hata wa vijijini kabisa, aweze kunufaika na juhudi za serikali katika kuimarisha kilimo.
“Nitoe rai kwa uongozi wa ITRACOM kuhakikisha mnaimarisha mfumo wa usambazaji wa mbolea hadi kwa wakulima waliopo vijijini ili waweze kuipata kwa gharama nafuu,” alisema Rais Samia huku akihimiza pia utoaji wa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea hiyo.
Akisisitiza juu ya umuhimu wa maarifa sahihi, Rais Samia alisema kuwa kufikisha mbolea pekee haitoshi, bali lazima elimu ya vipimo sahihi na matumizi kulingana na zao na aina ya udongo itolewe kwa wakulima na kwamba elimu hiyo itasaidia kuongeza tija, kupunguza umaskini, na kutoa ajira zaidi kwa vijana na wanawake, hatua itakayoiwezesha Tanzania kufikia malengo yake ya usalama wa chakula.
Katika hotuba yake, Rais Samia pia aligusia ushirikiano wa kikanda, akieleza kuwa biashara kati ya Tanzania na Burundi inaendelea kukua. Alisema, “Uwekezaji huu unaongeza fursa za ajira kwa vijana wetu, na kupitia mpango wa kuongeza vituo vya pembejeo, wakulima sasa wanapata vifaa kwa bei nafuu.”
Kwa upande wake, Rais wa Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimiye, alifurahishwa na hatua hiyo kubwa ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, akisema, “Zamani tulikuwa tunakuja Tanzania kama wakimbizi, sasa tunakuja kama wawekezaji.” Alisisitiza kuwa kiwanda cha ITRACOM hakitachangia tu maendeleo ya kilimo, bali pia kitaimarisha mshikamano wa kikanda Afrika Mashariki.
Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe, alieleza kuwa serikali ya awamu ya sita imewekeza kwa dhati katika sekta ya kilimo. Alisema zaidi ya shilingi bilioni 700 zimetengwa kwa ruzuku ya mbolea, huku bilioni 500 zikielekezwa kwa wakulima wa korosho. Alifichua pia kuwa kuanzia Septemba Mosi, 2025, wakulima watanunua mbolea kwa bei ya ruzuku—hatua inayolenga kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza tija kwa mkulima.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa ITRACOM, Bw. Nduwimana Nazaire, kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha tani milioni moja za mbolea kwa mwaka na tayari kimezalisha ajira zaidi ya 1,800 za moja kwa moja. Uzinduzi wa kiwanda hiki unaashiria mwelekeo mpya wa Tanzania katika mapinduzi ya kilimo, yakilenga si tu kuongeza uzalishaji, bali kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa ndani na ukanda mzima wa Afrika Mashariki.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.