Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi ya siku tano mkoani Ruvuma kuanzia Aprili 2, 2025, hadi Aprili 7, 2025.
Ziara hiyo inalenga kuimarisha chama, kuzungumza na wananchi, pamoja na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa CCM mkoa wa Ruvuma, John Foroteo Haule, Balozi Dkt. Nchimbi ataanza ziara yake kwa kupokelewa Wilayani Tunduru akitokea mkoa wa Mtwara.
Katika kipindi cha ziara yake, atatembelea Wilaya za Tunduru, Namtumbo, Mbinga, Nyasa na Songea Mjini, ambapo atafanya mikutano ya hadhara kwa lengo la kuzungumza na wananchi kuhusu utekelezaji wa Ilani ya CCM na kusikiliza changamoto zinazowakabili.
Mbali na mikutano hiyo, Katibu Mkuu wa CCM pia atakagua na kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo mradi mkubwa wa kimkakati wa ujenzi wa bandari ya Mbambabay wilayani Nyasa.
Ziara hii inatarajiwa kutoa fursa ya tathmini ya utekelezaji wa miradi hiyo na kuimarisha ushirikiano kati ya chama, serikali na wananchi katika kuwaletea maendeleo endelevu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.