Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, Ndg. Philemon Mwita Magesa, ameongoza ziara ya ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa vituo viwili vya afya katika vijiji vya Mchomolo na Mgombasi, wilayani humo.
Miradi hiyo yenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 508, inatekelezwa na mkandarasi DMC Contractor Limited, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuboresha huduma za afya katika maeneo ya pembezoni.
Mradi huo unatekelezwa kwa mujibu wa mkataba ulioanza tarehe 1 Julai 2025, na unatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 2025, ndani ya kipindi cha miezi mitatu. Ujenzi katika kituo cha afya cha Mchomolo unagharimu shilingi milioni 258, wakati ule wa Mgombasi ukigharimu shilingi milioni 250.
Fedha hizo zimetolewa na Serikali kupitia bajeti ya maendeleo ya sekta ya afya, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora na za karibu.
Katika vituo hivyo vinavyojengwa, miongoni mwa majengo yanayojengwa ni pamoja na jengo la huduma ya wagonjwa wa nje (PPD), pamoja na miundombinu mingine muhimu kama maabara, wodi za wagonjwa, nyumba za watumishi na vyoo vya kisasa. Mkurugenzi Magesa ameweka bayana kuwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kupunguza vifo vinavyotokana na kukosa huduma ya afya kwa wakati, hasa kwa akina mama na watoto vijijini.
Akiwa katika ukaguzi huo, Mkurugenzi Magesa aliwataka wakandarasi kuhakikisha wanazingatia viwango vya kitaalamu, muda wa utekelezaji, na ubora wa kazi kwa mujibu wa mkataba. “Serikali haitakubali mzaha kwenye miradi ya afya, tunahitaji kazi bora, kwa wakati, ili wananchi waanze kunufaika haraka iwezekanavyo,” alisisitiza Magesa mbele ya wananchi, viongozi wa vijiji na wataalamu wa afya waliokuwepo katika ziara hiyo.
Wananchi wa vijiji husika wameonesha furaha yao kwa maendeleo ya ujenzi huo, wakieleza kuwa wamekuwa wakitembea zaidi ya kilomita 15 kufuata huduma za afya katika maeneo ya mbali, hali iliyokuwa ikiathiri hasa wazee, wajawazito na watoto. "Tunamshukuru sana Rais Samia kwa kutuletea kituo cha afya, tumeumia sana kwa miaka mingi," alisema Bi. Theresia Nyagawa, mkazi wa Mchomolo.
Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo inaendelea kutekeleza mikakati ya kuongeza vituo vya afya na hospitali katika kata mbalimbali ili kufikia lengo la kila kata kuwa na kituo cha afya ifikapo mwaka 2027. Tayari halmashauri hiyo ina vituo vya afya vinavyofanya kazi 11 na vingine vinne vikiwa katika hatua za ujenzi, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia70 tangu mwaka 2020.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.