Barabara ya Mbinga-Mbambabay kufungua fursa mpya za kiuchumi Ruvuma
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema kukamilika kwa ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara ya Mbinga hadi Mbambabay yenye urefu wa kilometa 66 kunafungua fursa mpya za kiuchumi.
Mndeme alikuwa anazungumza wakati anafungua kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Ruvuma kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea mjini Songea.
“Niwahakikishie wananchi kuwa serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe.Dkt John Magufuli imedhamiria kukamilisha na kuunganisha maeneo mbalimbali ya Mkoa wetu kwa barabara za lami’’,alisema Mndeme.
Amesema barabara hiyo inafungua sekta ya usafiri na usafirishaji ukanda wa ziwa Nyasa hivyo kuhitimisha malengo ya serikali ya kufungua ushoroba wa Mtwara(Mtwara Corridor) na kuunganisha kwa urahisi na usafiri wa ndege kupitia kiwanja cha Ndege Songea na meli kupitia bandari ya Mbambabay ziwa Nyasa.
Mndeme amesisitiza kuwa kukamilika kwa mtandao wa barabara ya Mbambabay kumewezesha Mkoa wa Ruvuma kufunguka ambapo hivi sasa ajira na biashara zitaongezeka na kwamba hadi kufikia Desemba 2020,Mkoa ulikuwa na kilometa 9,321.38 za mtandao wa barabara.
Hata hivyo amesema kati ya kilometa hizo,Wakala wa Barabara Mkoa(TANROASDS) anahudumia na kutunza barabara zenye urefu wa kilometa 2,175.18.
Kwa upande wake Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Lazack Alinanuswe amezitaja barabara za Mkoa kuwa zina urefu wa kilometa 1,270.78 na barabara kuu zina urefu wa kilometa 925.10.
“Wakala wa barabara za vijijini na mijini TARURA wanahudumia barabara zenye urefu wa kilometa 7,146.2,hadi sasa Mkoa umefanikiwa kuongeza mtandao wa kilometa 800.48 sawa na asilimia 8.6 ya barabara zote za TANROADS na TARURA’’,alisema.
Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa nchini ambayo makao makuu ya wilaya zote yameunganishwa kwa mtandao wa barabara ya lami.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Januari 11,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.