Na Albano Midelo
Katika jitihada za kuboresha miundombinu ya barabara mkoani Ruvuma, Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) unatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 10.1 kwa kiwango cha lami katika Manispaa ya Songea.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Silivester Chinengo anasema Mradi huo unafadhiliwa na mpango wa TACTIC kupitia Benki ya Dunia,katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, ukiwa na lengo la kuboresha miundombinu na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika mji wa Songea na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.
Amesema Ujenzi wa mradi huo unafanywa na mkandarasi mzawa, M/S CHINA SICHUAN INTERNATIONAL COOPERATION CO LTD, kwa gharama ya shilingi bilioni 22.27 na kwamba Usimamizi wa mradi huo unafanywa na Mhandisi mshauri HOWARD CONSULTING LIMITED kwa gharama ya shilingi milioni 939.39.
“ Hadi sasa, mradi umekamilika kwa asilimia 87.53 na unatarajiwa kukamilika rasmi ifikapo tarehe 8 Juni 2025’’,alisema Mhandisi Chinengo.
Wananchi wa Songea wanatarajia kupata manufaa makubwa kutoka kwa mradi huu, ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama za usafirishaji, kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu, na kuboresha biashara na uchumi wa mji wa Songea.
Zaidi ya hayo, barabara hizi zitasaidia kupunguza msongamano wa magari na kuboresha usalama wa watumiaji wa barabara katika Manispaa ya Songea.
Meneja wa TARURA Mkoa anasisitiza kuwa, mradi huo ni sehemu ya mpango mpana wa kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali ya mkoa, hatua inayolenga kuinua ustawi wa wananchi kwa kuwezesha maendeleo endelevu.
Mradi huu unaonesha azma ya serikali katika kuhakikisha maendeleo ya miundombinu yanaendelea kushika kasi, huku wananchi wa Songea wakisubiri kwa hamu kukamilika kwa asilimia 100 ili waweze kunufaika kikamilifu na barabara hizi za kisasa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.