Ndani ya mandhari ya kuvutia ya Mkoa wa Ruvuma, linapatikana moja ya maajabu ya asili yasiyo na kifani – chanzo cha Mto Ruvuma, mto mkubwa unaotiririsha maji kupitia mikoa kadhaa na hatimaye kumwaga maji yake katika Bahari ya Hindi.
Chanzo hiki kiko katika milima ya Matagoro, Kusini mwa Songea Mjini, na kinapendezesha mazingira kwa kijani kibichi cha misitu ya mvua na sauti ya ndege pori. Kwa wakazi na wageni, ni sehemu ya utulivu, uzuri wa asili na historia inayovuka vizazi, huku kikihifadhiwa kwa njia ya asili bila kuathiriwa na shughuli za kibinadamu.
Kadri Mto Ruvuma unavyosafiri kupitia nyika na misitu, unafikia kipande cha kuvutia sana cha ardhi kinachojulikana kama Maporomoko ya Nakatuta, yaliyopo ndani ya Pori la Akiba Liparamba. wilayani Nyasa, Maporomoko haya yanajitokeza kwa kishindo cha maji kinachotua kwa nguvu kwenye miamba, yakitengeneza ukungu na mvuke unaovutia kama pazia la asili.
Hii ni sehemu ambayo asili imeamua kuonesha ubunifu wake wa hali ya juu – penye utulivu na kishindo kwa wakati mmoja.
Pori la Akiba Liparamba, linalozunguka chanzo na maporomoko haya, ni hazina ya kipekee kwa wanyamapori na mimea ya asili. Eneo hili linatunzwa na Serikali kwa lengo la kuhifadhi bioanuwai na vyanzo vya maji, huku likiwa kivutio kikuu kwa watalii na watafiti wa mazingira.
Wale wanaotembelea sehemu hii wanapata fursa ya kushuhudia uhusiano wa karibu kati ya maji, misitu, na viumbe hai katika hali yao halisi. Bila shaka, Mto Ruvuma na maporomoko ya Nakatuta ni miongoni mwa vivutio vya asili vinavyostahili kutangazwa duniani kote kama urithi wa pekee wa Tanzania.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.