MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Mheshimiwa Simon Chacha,amewataka Viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika(AMCOS)Wilayani humo,kuacha upendeleo kwenye ugawaji wa pembejeo za ruzuku zinazotolewa bure na Serikali ili kila mkulima aweze kunufaika na pembejeo hizo zinazotumika kwa ajili ya kupulizia mikorosho.
Amesema,hatua hiyo itajenga imani,kuleta mshikamano na kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima kati yao na wanachama wao wanaowaongoza.
Chacha amesema hayo,alipokuwa akizungumza na baadhi ya wakulima wanaohudumiwa na Chama cha msingi cha Ushirika cha Mtetesi AMCOS, baada ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa wakulima wa vijiji vinne vya Mtonya,Mindu,Liwangula na kitingoji cha Mjimwema wakilalamika kukosa mgao wa dawa aina ya Sulfa, hivyo kushindwa kuendelea na maandalizi ya kilimo cha zao la korosho katika msimu 2024/2025.
Amesema,iwapo viongozi ambao ni wasimamizi wa Amcos hizo watafanya shughuli kwa misingi ya upendeleo na kutanguliza maslahi binafsi ,basi juhudi za kufikia malengo kupitia sekta ya ushirika zitakwama.
Amesisitiza kuwa,ili malengo ya chama yaweze kufikiwa ni muhimu kwa viongozi wa Ushirika kufanya kazi kwa kufuata sheria,usawa,kutenda haki,uwazi na uwajibikaji na kukumbuka malengo ya kuanzishwa kwa Ushirika ili wanachama wapate mkombozi katika harakati za kupambana na umaskini.
Kwa upande wake Meneja wa Chama kikuu cha Ushirika(TAMCU ) wilayani humo Marcelino Mrope amesema,katika mapokeo ya Sulfa katika msimu wa kilimo 2024/2025 maghala matatu yamehusika ambayo ni ghala la Chama kikuu cha Ushirika,ghala la chama cha msingi Namiungo na Namitili Amcos.
Mrope,amekiri wakulima wa Chama cha Namitili na Namiungo AMCOS wamepata mgao wa Sulfa mara mbili ikilinganishwa na wakulima wa vijiji vingine kutokana na maghala yake kuwa na sifa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.