Diwani wa kata ya Likuyu Wilayani Namtumbo Mkoani Ruvuma Mheshimiwa Kassimu Gunda amewashauri viongozi wa Serikali Kuwajenga wananchi kisaikolojia kwenye migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Likuyu,Gunda amesema ipo tabia ya viongozi kutojitokeza kwenye migogoro kati ya wanyamapori na binadamu hasa inapotokea binadamu kuuawa na tembo kwa kuogopa Wananchi kuwa na hasira Kwa viongozi wao.
Gunda ameitaja faida ya viongozi kuwa na wananchi wakati wa matatizo yao kunawajenga wananchi kisaikolojia hivyo kushirikiana nao bega Kwa bega kwenye changamoto mbalimbali .
Diwani huyo ameiomba serikali Kuharakisha kifutajasho kwa wananchi pale wanapoathirika na tembo ili wananchi walioathirika na wanyamapori waweze Kununua chakula ambacho kiliharibiwa na wanyamapori hao.
Hata hivyo Menas Fusi Mkazi wa kitongoji cha Mfuate Kijiji Cha Likuyu amesema kasi ya tembo kwenda katika mashamba ya wakulima imepungua Kutokana na kuwepo Kwa Jeshi la TANAPA ambalo Kwa kiasi kikubwa hufanya kazi ya kuwarudisha tembo hao katika hifadhi .
Afisa Maliasili na Utalii wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo Priska Msuha amesema Licha ya kutokea Changamoto ya tembo mmoja mwenye mtoto kumua mwananchi katika Kijiji Cha Likuyu hivi karibuni, changamoto ya tembo imepungua Kutokana na Kambi ya TANAPA kufanya kazi kubwa ya kuwarudisha wanyamapori hao hifadhini.
Afisa Maliasili huyo amesema ofisi yake inaendelea kutoa elimu ya namna ya kukabiliana na wanyamapori kama tembo ambapo hivi sasa wananchi wakimwona tembo hawamfuati hubaki kimya badala yake wanapiga simu kwa Mamlaka zinazohusika ambao hufika kuwaondoa tembo hao katika makazi ya watu.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.