Na Albano Midelo
Katika bonde la kijani lililojaa mandhari ya kuvutia kusini mwa Tanzania, wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma sasa inang’aa kama nyota mpya ya utalii.
Kupitia uwekezaji wa Shilingi bilioni 2.1 kutoka Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, lango la kisasa kuingia Hifadhi ya Taifa ya Nyerere limejengwa eneo la Likuyuseka Maganga na sasa, ndio mlango rasmi wa watalii kuingia hifadhi hiyo kupitia Nyanda za Juu Kusini.
Akizungumza kwa furaha, Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo, Mheshimiwa Ngollo Malenya, anasema ujenzi wa lango hilo umekamilika na sasa wilaya yake ipo tayari kuwakaribisha wageni kutoka kila pembe ya ukanda wa kusini,ikiwemo mikoa ya Lindi, Mtwara, Njombe, Iringa, Mbeya hadi Ruvuma, na hata nchi jirani kama Msumbiji na Malawi.
“Lango hili ni fursa ya kipekee kwa Namtumbo na Mkoa wa Ruvuma. Linakuza uchumi wetu kwa haraka na linafungua njia ya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya utalii,” anasisitiza Malenya huku akitoa rai kwa wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza kwenye ujenzi wa hoteli, huduma za utalii na miundombinu mingine muhimu.
Mlango Mpya, Fursa Mpya
Lango la Namtumbo ni mojawapo ya njia muhimu za kuingia Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, mojawapo ya hifadhi kubwa zaidi Afrika inayochukua zaidi ya kilomita za mraba 30,000. Hifadhi hii ilianzishwa rasmi mwaka 2019, ikiwa sehemu ya urithi wa zamani wa Selous Game Reserve.
Kupitia lango hili, wageni kutoka mikoa ya kusini sasa wanaweza kufurahia urahisi wa kuingia hifadhi hiyo bila kupitia njia za mbali.
Wageni kutoka Songea, Tunduru na maeneo ya mpakani mwa Msumbiji wanaweza sasa kuingia moja kwa moja kwenye mbuga hiyo tajiri kwa wanyamapori na mandhari ya kuvutia.
Vivutio Vilivyo Karibu na Lango
Eneo hili linajivunia kuwa na wanyamapori wakubwa kama tembo, simba, chui, nyati, na pundamilia wanaoonekana mara kwa mara katika maeneo ya karibu na lango.
Kivutio kingine ni bwawa la Kaunde, linalofahamika kama bwawa la viboko.Ni bwawa la pekee, lililoko juu ya mlima, na lenye sifa ya kushangaza, maji yake hayakauki mwaka mzima, lakini chanzo chake hakijulikani.
Likiwa limezungukwa na milima na msitu mnene wa hifadhi, bwawa hili limebaki kuwa eneo la asili lisiloguswa, kivutio kwa watalii wa ndani na wa kimataifa wanaotafuta uzuri wa Tanzania.
Isitoshe, Namtumbo inaongeza thamani ya utalii kupitia vivutio vya kiutamaduni. Watalii wanaweza kutembelea vijiji vya Wandendeule na Wangoni na kujifunza historia, mila na utamaduni wa watu wa Ruvuma.
Matokeo kwa Jamii
Kwa jamii ya Namtumbo, faida tayari zimeanza kuonekana. Vijana wameanza kupata ajira kama waongoza watalii, madereva, wapishi na wahudumu wa hoteli. Wananchi pia wanashiriki kwenye miradi ya ujirani mwema inayoratibiwa na TANAPA,TAWA na TFS.
Kwa uwepo wa lango la kisasa la Namtumbo, si tu kwamba Ruvuma imejiunga rasmi na ramani ya utalii wa kimataifa, bali pia imepiga hatua kubwa katika kujenga uchumi shirikishi unaowagusa watu wa kawaida.
Karibu Namtumbo,mlango wa kusini unaofungua milango ya fursa za utalii na uwekezaji zisizo na kikomo.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.