Hifadhi ya msitu wa Wino iliyopo katika Halmashauri ya Madaba wilayani Songea mkoani Ruvuma ni miongoni mwa mashamba 24 ya miti ya kupandwa yanayosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania
Hifadhi hii kwa sasa ina ukubwa wa hekta 39,718 zinazoundwa na safu tatu (Wino 2,259ha, Ifinga 29,000ha na Mkongotema 8,459ha).
Mhifadhi Mkuu wa Shamba miti Wino Glory Kasmiri anasema uhifadhi ya msitu wa Wino ulianza kuendelezwa na TFS mwaka 2010 ikihusisha eneo dogo la msitu wa asili wenye ukubwa wa hekta 2,259 (ambayo ndio safu ya Wino).
“baadae mwaka 2014 na 2016 tulipata maeneo kutoka vijiji vya Mkongotema na Ifinga , tangu tumeanza upandaji wa miti mpaka sasa jumla ya hekta 5,495 zimepandwa miti ya jamii mbalimbali lakini sehemu kubwa ikiwa ni misindano’’,anasema Kasimir
Anabainisha kuwa shamba la miti Wino limeendelea kuboresha mahusiano na wananchi,na kwamba katika kutekeleza hayo Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kupitia Shamba la miti Wino uliridhia na kufadhili mradi wa maji kijiji cha Ifinga uliogharimu Zaidi ya milioni 482.
Ametoa rai kwa wananchi na jamii kutunza mradi huu na maeneo yote ya vyanzo vya maji ili kuhakikisha upatikanaji wa maji unakuwa endelevu.
Anayataja malengo makuu ya kuanzishwa kwa Hifadhi ya msitu wa Wino ni pamoja na:Kuhifadhi maliasili zinazotaka kutoweka na vyanzo vya maji, Vyanzo vya mto upahila – lutukila-luhuhu-Ziwa Nyasa,Mto Mnywa masi – Pitu-Ruhuji-ifakara-Rufiji,Mto Mwesa – Ruhuji na Mto Lutukila – Luhuhu.
Mito mingine ni Mgombezi – Lutukila,Mto Kineneka – Lutukila,Mto Kipilili – Pitu,Mto Balali – Pitu,Mto Mapancha – Chechengu-pitu,Mto Mbega – Chechengu na Mto Chechengu – Pitu
Malengo mengine ya kuanzishwa kwa shamba hilo ameyataja kuwa ni kutoa ajira kwa Watumishi wa kudumu 15, mkataba 10, vibarua wa msimu wanakadiriwa kufikia 4,000,Mazao ya biashara kama mbao na nguzo za umeme kwa siku za usoni ili kuongeza mapato ya serikali n Kuboresha mazingira na hali nzuri ya hewa . Akizungumzia shughuli za upandaji miti katika Shamba la miti Wino,Meneja huyo anasema upandaji miti unaeendelea kufanyika kwa lengo la kuhakikisha uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji vinatunzwa vizuri kwa upatikanaji maji na mazao ya Misitu kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Hata hivyo ameitaja changamoto ya matukio ya moto kwa kiasi kikubwa hupunguza jitihada za usimamizi endelevu wa shamba. Vyanzo vikuu vya moto ni uandaaji wa mashamba msimu wa kilimo kwa kutumia moto ambapo kwa mwaka 2016 ziliungua hekta 600 na 2021 hekta 1,623 ukisababishwa na uaandaaji wa mashamba maeneo ya mabonde yanayopakana na Shamba.
Katika kukabiliana na tatizo hili, Uongozi wa Shamba la miti wino umekuwa ukitoa elimu na vifaa vya kuzimia moto kwa jamii,kutoa msaada wa vitendea kazi vinavyotumika kuzimia moto kwa jamii,kujenga mahusiano mema na vijiji vinavyozunguka Shamba kwa kuwapatia vifaa vya ujenzi mbalimbali.
Hatua nyingine zinazochukuliwa amezitaja kuwa ni kufanya kazi za kinga dhidi ya moto (kusafisha Fire lines na kufungua barabara, Kufyekea miti, uwepo wa vituo 3 vya mawasiliano, doria ya msituni mwaka mzima, kuimarisha ulinzi wa kupambana na moto kipindi chote cha kiangazi, kuweka gari standby kwa kiangazi na mfumo wa satelaiti wa kuangalia matukio ya moto uliopo makao makuu ya Wakala.
“Shamba la miti Wino linaendelea kuwaomba wananchi kuepuka kuanzisha moto maeneo hatarishi wakati wa uandaaji wa mashamba na kuwataka kufanya maandalizi mazuri ya barabara za kinga moto’’,anasema.
Licha ya changamoto hizo Shamba la Miti Wino limeweza kufanikiwa kuhifadhi eneo,miti iliopandwa imestawi vizuri,TFS kupitia shamba hili imeimarisha ushirikiano wake na jamii na uongozi katika ngazi mbalimbali,shamba limetoa ajira miaka yote kwa makundi mbalimbali. Kwa wastani wananchi 4,000 hujipatia ajira za mda mrefu na mfupi katika shamba hili kwa mwaka.
Anasema shamba hilo pia limevutia wawekezaji wengine kuja eneo hili,kikiwemo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambapo pia wamepewa ardhi na kijiji cha Ifinga.
Anaitaja mipango ya baadaye ya shamba hilo ni kuhakikisha kwamba mazingira yanatunzwa ipasavyo na upatikanaji wa malighafi kwa viwanda vya misitu na watumiaji wengine unakua endelevu kwa kizazi kilichopo na kijacho.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.