Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amefungua Jukwaa la kuimarisha uhifadhi ushoroba wa Selous Niassa ambalo limefanyika kwa siku mbili kwenye ukumbi wa Heritage Cottage mjini Songea.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Jukwaa hilo Mndeme amewaagiza wadau wa uhifadhi mkoani Ruvuma kuhakikisha kuwa ushoroba wa wanyamapori wa Selous Niassa unaimarika na kufikia malengo ya kunufaisha jamii za kizazi cha sasa na kijacho.
“Eneo la ushoroba wa Selous Niassa limebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa rasilimali mbalimbali za mimea,wanyamapori,ndiyo maana Pori la Akiba la Selous limechaguliwa na UNESCO kuwa urithi wa dunia na kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere’’,alisema Mndeme.
Amesema ushoroba huo una makundi makubwa ya wanyamapori kama tembo,mbwamwitu,nyati,viboko na simba na kwamba ushoroba huo ni muhimu kwa hifadhi mbili za Tanzania na Msumbiji yaani Selous na Niassa.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa,sekta ya utalii nchini inaingiza pesa nyingi za kigeni kwa kuwa inaleta wageni milioni 1.5 kwa mwaka na kwamba utalii pekee unachangia pato la Taifa kwa asilimia 17 na kutoa ajira kwa watanzania milioni mbili.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Uwanda wa Ruvuma wa Shirika la WWF Diana Shuma amesema jukwaa hilo la Mkoa ni la pili kufanyika likihusisha ushoroba wa Selous Niassa na kwamba kikao hicho kinawakutanisha wadau ili kujadili namna ya kuhifadhi ushoroba huo ambao upo katika hatari ya kutoweka.
Amesema ushoroba huo ni muhimu kwa Tanzania na Msumbiji kwa kuwa ni mapitio muhimu ya wanyamapori na unakabiliwa na changamto ya watu kufanya shughuli za kiuchumi ikiwemo kilimo na ufugaji.
“Lengo la kuanzisha jukwaa hili ni kuwaleta pamoja wadau kujadili na kutengeneza mikakati ya kuhifadhi ushoroba huu wa Selous Niassa ambao una ukubwa wa hekta zaidi ya milioni 1.5’’,alisisitiza Shuma.
Fidel Kimario ni Mratibu Uhifadhi Wanyamapori na mapito ya wanyama Wizara ya Maliasili na Utalii amesema serikali imeandaa kanuni za kusimamia mapito ya wanyamapori ili kukabiliana na hatari ya kutoweka mapito ya wanyamapori.
Enock Msocha ni Kaimu Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Kanda ya Kusini Mashariki wa TAWA inayohusisha mikoa ya Lindi,Mtwara na Ruvuma,amesema wameongeza mbinu mbalimbali za kulilinda pori la Selous ikiwemo kuongeza doria katika maeneo yote wakati wote.
Hata hivyo amesema wanashirikiana na wananchi katika maeneo jirani ya hifadhi kufanya ulinzi na kufuatilia wanyama kwa karibu endapo wamevuka katika maeneo ya wananchi ili wananchi na wanyama waweze kuwa salama.
Imendikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Desemba 11,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.