Tume ya Utumishi wa Mahakama imetoa mafunzo mkoani Ruvuma kwa wajumbe wa Kamati za Maadili ya Mahakama Ngazi ya Mkoa na Wilaya ya Songea yakiwa na lengo la kuongeza uelewa na ujuzi kwa viongozi na maafisa wa Mahakama waliopo katika kamati hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati hiyo ngazi ya mkoa, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, akifungua mafunzo hayo ambayo yamefanyika katika ukumbi wa Mipango uliopo katika ofisi yake mjini Songea, amesema mafunzo hayo yanaongeza uelewa kwa viongozi na kuwakumbusha maafisa wa Mahakama namna wanavyotakiwa kuwahudumia wananchi.
Ameongeza kuwa kamati hizo zimetayarishwa kwa ajili ya kupokea malalamiko ya wananchi dhidi ya mahakimu ngazi ya mkoa na wilaya ambao watakuwa wamefanya makosa ya kimaadili, kutekeleza majukumu yao kwa uzembe au kukiuka maadili ya mahakimu pamoja na mwenendo mbaya katika jamii.
Naye Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Songea, Mhe. James Karayemaha, amesema mafunzo hayo ni muhimu pia ni dira ya kuwaonyesha wanapoelekea kwa kuwa yatawasaidia kujua namna ya kufanya kazi zao kwa weledi, uaminifu na namna ya kuwajibika.
Kwa upande wake Naibu Katibu Maadili na Nidhamu Tume ya Utumishi wa Mahakama, Alexia Mbuya, amesema changamoto kubwa ni wananchi kutojua uwepo wa kamati hizo hivyo wenyeviti wa kamati za maadili ya Mahakama kwa Mkoa na Wilaya wawasaidie kutoa Elimu kwa wananchi wanapokuwa katika mikutano ya hadhara ili wapate uelewa juu ya uwepo wa kamati hizo na majukumu wanayotekeleza.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bi. Mary Makondo, amesema wao kama wajumbe wa kamati hizo katika ngazi ya mkoa na wilaya mafunzo hayo yanawapatia uelewa mkubwa na nuru kubwa kwa ajili ya kuwajibika.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.