WIZARA ya Afya kwa kushirikiana na kitengo cha kifua kikuu na ukoma Hospitali ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma,imeendelea na kampeni ya upimaji wa maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu kwa wananchi katika maeneo ya vijijini wilayani humo.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Masonya wakati wa kampeni za uelimishaji,uibuaji na uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu, Muhudumu wa afya ngazi ya jamii Menrad Hyera alisema,lengo la kampeni hizo ni kuhakikisha wananchi wanakuwa salama bila maambukizi ya ugonjwa huo unaotajwa kuwa miongoni mwa magonjwa kumi yanayopoteza watu wengi hapa nchini.
Alisema,kutokana na ukubwa wa tatizo la kifua kikuu hapa nchini, ndiyo maana serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau Shirika la Amref Health Africa na DMH wanaendelea na mapambano ya kutokomeza ugonjwa huo ili jamii iwe salama na kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Alisema,ugonjwa wa kifua kikuu unatibika na huduma zake zinatolewa bure katika vituo vyote vya kutolea huduma,Hospitali binafsi na serikali hapa nchini na kuwataka wananchi kuwa na tabia ya kufanya uchunguzi wa afya zao mara kwa mara ili kubaini kama wameambukizwa TB.
Ametaja dalili za kifua kikuu kwa watu wazima ni kupungua uzito,kutokwa na jasho jingi nyakati za usiku,kukohoa zaidi ya wiki mbili,kukohoa makohozi yaliyochanganyika na damu na kwa watoto kulilia,kukosa raha na makuzi duni.
Amewaonya wananchi,kuacha tabia ya kumeza dawa bila kupata ushauri wa kitaalam au kukimbilia kwa waganga wa tiba asili na tiba mbadala kila wanapohisi kuwa na homa,badala yake kwenda katika vituo vya kutolea huduma ili kufanya uchunguzi wa afya zao.
Hyera,amewashauri kufuata na kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalam wakiwemo wahudumu ngazi ya jamii wanaopatikana katika maeneo yao ili kuepuka kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali ikiwemo kifua kikuu.
Hyera ameitaka jamii, kuwa na mahusiano ya karibu na wahudumu wa afya ngazi ya jamii waliopo katika maeneo yao wenye jukumu la kukusanya sampuli za makohozi na kuzipeleke kwenye vituo vya kutolea huduma na Hospitali kwa ajili ya uchunguzi.
Kwa upande wake Mratibu na mdhibiti wa kifua kikuu kutoka shirika la Amref-Health Africa Lilian Ishengoma alisema,lengo la kampeni hiyo ni kuwafikia wagonjwa wote waliopo katika jamii ili kuwaanzishia matibabu na kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo.
Ishengoma,amepongeza jitihada zinazofanywa na Hospitali ya wilaya ya Tunduru kitengo cha kifua kikuu na ukoma kwa kazi nzuri katika kutokomeza ugonjwa huo na kutaka maeneo mengine kuiga ili kwa pamoja nchi yetu ibaki salama bila maambukizi ya kifua kikuu.
Mkazi wa kijiji cha Masonya Ahmad Halfani,ameishukuru serikali kwa kufanya kampeni hizo kwani zinasaidia sana wananchi kupata uelewa kuhusu ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma na kufanya uchunguzi na kufahamu hali za afya zao.
Hata hivyo,ameiomba Serikali kuendelea kufanya kampeni hizo mara kwa mara ili kuwafikia watu wengi, kwani ugonjwa wa kifua kikuu upo na watu wengi wanaugua bila kupata tiba sahihi jambo lililochangia baadhi ya familia kukosa nguvu kazi na kukabiliwa na umaskini.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.