KAYA zipatazo 110 zinazoishi kwenye mazingira magumu na hatarishi katika kata ya Ruvuma Manispaa ya Songea,zimepatiwa msaada wa vifaa vya kufukuza mbu majumbani (Mosquito fans) sambamba na kupatiwa elimu kuhusu matumizi sahihi ya vifaa hivyo na chandarua.
Vifaa hivyo, vimetolewa na kampuni ya Afrika Power kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Children of Songea kwa ajili ya kuwakinga wananchi hasa watoto wadogo wanaishi kwenye mazingira magumu dhidi ya ugonjwa wa malaria.
Akizungumza wakati wa kugawa vifaa hivyo,mwakilishi wa kampuni ya Afrika Power ya Dar es slaam Najumo Kipepe alisema,suala la afya ni muhimu na wameamua kugawa vifaa hivyo ili wananchi wavitumie katika kukabiliana na ugonjwa wa malaria ambao unatajwa kuwa miongoni mwa magonjwa yanayopoteza maisha ya watu wengi hapa nchini.
Kipepe alisema,kampuni ya Afrika Power inajali na kuthamini sana eneo la afya za wananchi ndiyo maana imetoa vifaa kwa kutambua kuwa kata ya Ruvuma ni miongoni mwa maeneo yenye idadi kubwa ya watu wanaoishi kwenye mazingira magumu na yako katika hatari ya kupata magonjwa mbalimbali.
Kwa mujibu wa Kipepe,vifaa vina thamani ya Sh.milioni tano na ni mwendelezo wa kampuni hiyo kutoa misaada mbalimbali kwa jamii hasa yenye mahitaji maalum wakiwamo watoto wanaosoma kwenye shule za msingi na sekondari.
Aliongeza kuwa, mwezi uliopita walitoa msaada wa umeme jua(solar)ili kuwawezesha watoto kupata muda wa kujisomea hata nyakati za usiku na waweze kufanya vizuri katika masomo na mitihani yao.
“kwa hiyo tumekuja kata ya Ruvuma mkoani Ruvuma kugawa vifaa hivi ili visaidie jamii ya apa hasa wanafunzi ili kuimarisha afya zao na kuhakikisha jamii yote inakuwa na afya njema kwa kuepukana na malaria”alisema Kipepe.
Alisema,kazi kubwa inayofanyika ni kuunga mkono juhudi mbalimbali za serikali katika kutokomeza maradhi mbalimbali na wanafunzi wanapata nafasi na muda wa kujisomea ili waweze kufanya vizuri katika safari yao ya masomo.
Mwakilishi wa Shirika la Children of Songea Ester Zenda alisema,kazi kubwa inayofanywa na shirika hilo ni kusaidia watu wanaoishi katika mazingira magumu na watoto yatima katika Manispaa ya Songea.
Alisema,awali walipofika kwa mara ya kwanza walielezwa kuhusu ukubwa wa tatizo la ugonjwa huo katika kata ya Ruvuma ambapo kwa kushirikiana na serikali za mitaa wamefanikiwa kupata angalau watoto 110, hata hivyo wanashindwa kuwafikia watu wote kutokana na kuwepo kwa watu wengi wanaohitaji msaada.Alisema,wamelipia gharama za matibabu kupitia mfuko wa afya ya jamii(CHF)ili watoto hao wawe na uhakika wa kupata matibabu pindi wanapougua na kuwaomba wadau wengine kujitokeza na kuungana nao ili kwa pamoja waweze kuwasaidia watu wenye mahitaji.
Naye muhudumu wa afya ngazi ya jamii kutoka kata ya Ruvuma Asia Milanzi alisema, ni vyema jamii ikakumbuka kutumia chandarua mara kwa mara wakati wa kulala ili kupata ugonjwa wa malaria ambao ni tishio kwa jamii nyingi za Kitanzania.
Amewahimiza kuhakikisha wanakula vyakula bora ili kuepuka uwezekano wa kupata na ugonjwa huo ambao unachangia kwa kiwango kikubwa tatizo la umaskini.
Alisema,kwa kawaida mtu anayeugua malaria na magonjwa mengine kuna uwezekano mkubwa wa kuleta umaskini ndani ya familia kwa sababu hana uwezo wa kufanya kazi za kuleta kipato.
Alisema,kama muhudumu wa afya ngazi ya jamii atahakikisha wananchi wa eneo hilo wanaendelea kupata elimu juu ya matumizi sahihi ya vyandarua ili wasipate malaria na kuathiri afya zao.
Afisa Mtendaji wa kata ya Ruvuma Beatrice Kapinga amelishukuru shirika la Children of Songea kufika katika kata hiyo na kutoa misaada mbalimbali kwa watoto wanaotoka katika kata hiyo ambayo itasaidia kujikinga na maradhi mbalimbali na kupata muda wa kujisomea.
Akizungumza kwa niaba ya watoto wenzake Salkha Njelekela mwanafunzi wa kidato cha kwanza shule ya sekondari Matogoro alisema,vifaa hivyo vitawasaidia kujikinga na ugonjwa wa malaria na kuongeza hamasa ya kujisomea hasa nyakati za usiku.
MWISHO.
ReplyReply allForward |
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.