Katika kikao kazi maalum kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Jiji la Dodoma, Mji wa Serikali Mtumba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ametoa maagizo makubwa kwa Maafisa Habari wa Mikoa, Halmashauri na Taasisi chini ya OR-TAMISEMI, akisisitiza kuwa wao ni kiungo muhimu katika kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya nchi.
Akizungumza kwenye kikao kazi hicho, Mchengerwa amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri na makatibu Tawala wa mikoa kuhakikisha Maafisa Habari wanapewa nafasi ya kushiriki kikamilifu kwenye kila hatua ya maendeleo.
Mchengerwa ameweka bayana kuwa Maafisa Habari si watazamaji bali ni sehemu ya timu ya maendeleo, hivyo lazima wahusishwe katika ziara za viongozi, tathmini za miradi na kikao chochote rasmi.
“Maafisa Habari wakiwa na uelewa mpana wa yanayotekelezwa, watakuwa na nguvu ya kusambaza habari sahihi kwa umma na kuijenga Serikali kwa msingi wa uwazi,” amesema Waziri huyo kwa msisitizo.
Katika kuhakikisha weledi wa Maafisa Habari unaimarishwa, Mchengerwa ametoa agizo kwa Wakurugenzi na Makatibu Tawala kuandaa mafunzo kazini kwa watumishi hao, yakiwemo uandishi wa takwimu, ubunifu wa infographics, uhariri wa video, na maudhui mengine ya kisasa ya mawasiliano.
Aidha, ametilia mkazo umuhimu wa kuwahusisha Maafisa Habari katika vikao vyote vya kisheria na kuwawezesha kuwa sehemu ya menejimenti rasmi.
Waziri Mchengerwa pia amewataka viongozi wa Mikoa na Halmashauri kuhakikisha kila Afisa Habari anapatiwa ofisi yake, bajeti maalum ya uendeshaji, na kushirikishwa katika kuratibu vipindi vya televisheni na redio vinavyoitangaza Serikali. “Fedha zipo, lakini hazitumiwi ipasavyo kwenye mawasiliano. Hili halikubaliki,” alisisitiza kwa ukali.
Kwa upande wao, Maafisa Habari wametakiwa kuandaa Mpango Kazi unaoendana na vipaumbele vya taasisi zao, kuwasilisha taarifa za utendaji kila baada ya miezi mitatu, na kuwa wabunifu katika uchakataji na usambazaji wa habari.
Waziri amesisitiza kuwa mitandao ya kijamii na tovuti rasmi ni nyenzo kuu ya kufikisha taarifa kwa wananchi, hivyo inapaswa kuhuishwa kila wakati.
Kikao hicho kimeweka msingi wa mageuzi makubwa katika mfumo wa mawasiliano ya Serikali, huku Mchengerwa akisisitiza kuwa kila Afisa Habari anapaswa kuwa “shujaa wa simulizi ya maendeleo”.
Ametaka taarifa zote za miradi ya maendeleo zifuatiliwe kwa karibu ili wananchi wapate taarifa sahihi za utekelezaji wa miradi yao. “Tumeingia zama mpya – zama za Serikali ya uwazi, uwajibikaji na mawasiliano yenye mvuto kwa umma,” amehitimisha.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.