MKUU wa mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge,amekagua Daraja la Mto Muhesi wilayani Tunduru na kuiagiza wakala wa Barabara Tanroads mkoa huo, kusimamia matumizi sahihi ya mizani na kuwachukulia hatua kali madereva wanaozidisha uzito kwenye magari na baadhi ya watu wanaoiba na kuharibu kwa makusudi alama za barabara.
Brigedia Jenerali Ibuge,ametoa agizo hilo alipotembelea daraja la Mto Muhesi wilaya ya Tunduru ambalo baadhi ya miundombinu yake imeharibika baada ya kufunikwa na maji kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha wilayani humo na mikoa jirani.
Mkuu huyo wa mkoa,amemuagiza meneja wa Tanroads mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ephatar Mlavi kufanya tathimini ya athari iliyotokea na kufanya matengenezo ya haraka kwa kuwa daraja hilo ni muhimu kwa uchumi wa Ruvuma na mikoa mingine ya Lindi na Mtwara ili wananchi waendelee na shughuli zao za maendeleo.
Amewataka,madereva wanaoendesha magari ya abiria na malori kuzingatia sheria kwa kuepuka kuzidisha uzito ili kulinda barabara na miundombinu yake inayojengwa kwa gharama kubwa na Serikali.
Alisema, barabara ya Songea-Namtumbo hadi Tunduru ina muda mfupi takribani miaka mitano tangu ilipojengwa,lakini baadhi ya maeneo imeanza kuharibika na hali hiyo inatokana na madereva wasiozingatia sheria kwa kuzidisha uzito katika magari yao.
Aidha ameiomba Wizara ya ujenzi na Uchukuzi kupitia wakala wa Barabara Tanroads makao makuu, kujenga mizani nyingine kati ya Songea na Tunduru ili kudhibiti uzito wa magari.
Alisema, sehemu kubwa ya barabara hiyo hakuna udhibiti wa uzito wa magari badala yake kutegemea mizani ya Makambako na Tunduru tu ambazo zinatoa nafasi kwa madereva wasio waaminifu kuongeza mizigo njiani tofauti na ile iliyokaguliwa kwenye mizani hizo.
Ibuge,amewataka wananchi wa mkoa wa Ruvuma na watumiaji wengine wa barabara hiyo kuzingatia sheria na kuepuka kufanya shughuli za kibinadamu kando kando ya barabara kwani tabia hiyo inachangia sana kuharibu miundombinu ya barabara.
Brigedia Jenerali Ibuge,amempongeza Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro na meneja wa Tanroad mkoa kwa hatua walizochukua kuzuia magari na watu kupita kwenye daraja hilo kwani uamuzi huo umesaidia kuzuia kutokea kwa madhara makubwa.
Kwa upande wake Meneja wa Tanroads mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ephatar Mlavi alisema, baada ya kufanya ukaguzi wamebaini kipande kimoja cha daraja kimetoka sehemu yake,lakini wameruhusu kutumika kwa upande mmoja ili kutoa nafasi kwa wananchi kuendelea na shughuli zao.
Mlavi alisema, wameshatoa taarifa makao makuu ambapo vifaa na wataalam wameanza safari ya kuja eneo hilo kwa ajili ya kufanya marekebisho kipande kilichohama.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro alisema, mvua zilizonyesha katika mikoa ya jirani zilileta maji mengi katika Mto Muhesi na kusababisha daraja hilo kufunikwa na maji hali iliyosababisha usafiri kati ya mikoa ya Lindi,Mtwara kuelekea Ruvuma kusimama kwa muda.
Kwa mujibu wa Mtatiro,baada ya maji kupungua kamati ya ulinzi na usalama na ofisi ya Tanroads kufanya ukaguzi wa kina wameruhusu daraja hilo kutumika huku wakisubiri wataalam kwenda kufanya marekebisho ya kipande kilichoathirika.
Alisema,barabara ya Songea-Namtumbo-Tunduru hadi Mangaka mkoa jirani wa Mtwara mizani inayotumika kudhibiti uzito wa magari iko Tunduru tu jambo linalotoa nafasi kwa madereva wasiotaka kutii sheria kuongeza mizigo njiani,jambo lililochangia sehemu ya barabara hiyo kuanza kuharibika haraka.
MWISHO.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.