WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Halmashauri zote nchini waweke mpango wa namna bora ya kuviwezesha vikundi vya wajasiriamali katika maeneo yao kupitia mikopo ya asilimia 10 ya makusanyo ya ndani ambayo itawawezesha kuendeleza miradi yao na kuleta tija.
“Badala ya kutoa mikopo ya fedha kidogo kidogo mnaweza kutoa fedha nyingi kwenye kikundi kimoja kimoja kama shilingi milioni 200 kukiwezesha kikundi husika kuanzisha mradi mkubwa ambao unaweza kuwaingizia fedha nyingi hivyo kuongeza tija”
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amemtaka Meneja wa TARURA mkoa wa Ruvuma ashirikiane na Meneja wa TARURA wa wilaya ya Mbinga kufanya tathimini ya mahitaji ya matengenezo ya mtandao wa barabara katika maeneo ya uchimbaji wa makaa ya mawe na kuhakikisha zinapitika wakati wote ili kuwawezesha wawekezaji kufanya shughuli zao kwa ufanisi.
Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Januari 7, 2023) baada ya kutembelea na kukagua shughuli za uchimbaji wa makaa ya mawe katika mgodi wa kampuni ya Jitegemee Holdings ulioko katika kijiji cha Mdunduwalo, Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma.
Waziri Mkuu amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji hivyo ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lihakikishe linafikisha umeme wa gridi ya Taifa katika migodi ya makaa ya mawe mkoani Ruvuma ili kuwapunguzia wawekezaji gharama za uendeshaji.
Akizungumza baada ya kutembelea kampuni ya makaa ya mawe ya Jitegemee holdings, Waziri Mkuu amezitaka Jumuiya za Chama cha Mapinduzi wilaya ya Mbinga kuwekeza katika utengenezaji wa nishati ya mkaa wa kupikia kwa kutumia makaa ya mawe ili kudhibiti ukataji wa misitu na kuhamasisha utunzaji wa mazingira.
Amesema kuwa Chama cha Mapinduzi kimetoa msisitizo na muelekeo wa uwekezaji ndani ya Chama ambao utawezesha kujiendesha kwa kujiongezea kipato. “Tumieni fursa ya uwepo wa makaa ya mawe kwa kuanzisha viwanda vya kutengeneza mkaa wa kupikia kwa kutumia vumbi la makaa ya mawe na hivyo kujiongezea kipato.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Jitegemee Holdings, Emmanuela Kaganda amesema shughuli za uzalishaji katika mgodi zilianza rasmi Mei 2021 na una uwezo wa kuzalisha tani 2,500 hadi 3,000 za makaa ya mawe kwa siku kwa mashine zilizopo kwa sasa. Hadi kufikia Desemba 2022, jumla ya dani 652,128.8 za makaa ya mawe zimevunwa.
“Hadi kufikia Mwezi Desemba 2022 kampuni imeshauza jumla ya tani 522,450.08 za makaa ya mawe kwa wateja wa ndani na nje ya nchi. Kampuni imefanikiwa kusafirisha makaa ya mawe meli moja ya tani 22 kwenda nchini Congo DRC na mwezi huu wa Januari 2023 kampuni itasafirisha meli mbili za makaa ya mawe kwenda nje ya nchi. Meli moja ya tani 25,000 tayari ipo bandari ya Mtwara itaelekea Congo DRC na meli ya pili imeshafika nayo inapakia tani 55,000 za makaa kuelekea nchini Polland.”
Amesema kampuni yao imefanikiwa kuchangia shilingi bilioni 7.01 katika pato la Taifa, kati yake shilingi milioni 81.73 zimelipwa kwa halmashauri kupitia tozo na ushuru mbalimbali na Shilingi Milioni 292 ni kodi nyingine za serikali ikiwemo PAYE, kodi ya zuio na SDL.
“Kampuni imeshalipa Mrabaha jumla ya kiasi cha Shilingi Bilioni 3.59 na shilingi milioni 488 kama ada ya vibali vya kusafirisha mkaa nje ya nchi kuanzia Juni 2021 hadi Disemba 2022.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amekipongeza kikundi cha Mbalawala Women group kilichopo Ruanda, Wilaya ya Mbinga Mkoa wa Ruvuma ambacho kinajihusisha na utengenezaji wa mkaa wa kupikia kupitia makaa ya mawe na kwamba Serikali itaendelea kuwasaidia ili kuhakikisha wanaendelea na uzalishaji huo ambao ni muhimu katika utunzaji wa mazingira
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.