BARAZA la madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Songea limesikitishwa na wasimamizi wa Idara ya Elimu kushindwa kusimamia taaluma na kusababisha Halmashauri hiyo kushika mkia kati ya Halmashauri nane za Mkoa wa Ruvuma kwenye matokeo ya darasa la saba 2020.
Matokeo ya mtihani wa Taifa wa Darasa la saba 2020,yanaonesha kuwa Halmashauri hiyo ilifaulisha kwa asilimia 66.66 hivyo kuwa ya mwisho kimkoa.
Akizungumza kwenye mkutano wa Baraza la madiwani,Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Menas Komba ameiagiza Idara ya elimu msingi na sekondari kuanza kuchukua hatua kwa wasimamizi na walimu ambao hawafanyikazi.
“Sisi kama Baraza la madiwani sasa tutashughulika nao,tunataka Halmashauri ya Songea kielimu tuwe juu,serikali imetoa fedha za utoaji wa elimu bure,waratibu elimu kata wamepewa pikipiki,wanalipwa posho za madaraka shilingi 250,000 kila mwezi,wakuu wa shule za msingi wote wanalipwa posho za madaraka hawafanyi kazi kikamilifu’’,alisisitiza Komba.
Ametoa rai kwa maafisa elimu na wanaohusika kuchukua hatua na kwamba wanaoshindwa kusimamia elimu ameshauri wasihamishwe badala yake washushwe vyeo na kwa kutoa mapendekezo kwa Mkurugenzi na kuletwa kwenye kikao cha madiwani ili kushughulika nao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu,Afya na Maji katika Baraza hilo Manfred Mzuyu amesema kamati yake ilifanya utafiti kwa kutembelea kata,baada ya matokeo mabaya ya elimu ya msingi na kubaini kuwa baadhi ya waratibu elimu kata, pikipiki walizopewa na serikali wanazitumia kwa matumizi yao na hawaishi kwenye vituo vyao vya kazi.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kizuka Jacob Nditi amesema,uchunguzi walioufanya wamebaini wasimamizi wa elimu wakiwemo waratibu Elimu Kata na walimu wakuu baadhi yao hawasimami walimu ili kujua iwapo walimu wanafundisha ipasavyo.
“Kwanini baadhi ya waratibu hawaishi kwenye vituo vyao vya kazi,sababu ni nini zinazosababisha kupata ufaulu wa chini sana na kusababisha Halmashauri yetu kupata aibu’’,alihoji Diwani Nditi.
Naye Diwani wa Kata ya Mpitimbi Issa Said Kindamba amesema iwapo walimu wangewajibika ipasavyo darasani kwa usimamizi wa walimu wakuu,Halmashauri isingepata ufaulu wa hatari na kusababisha Halmashauri kushika nafasi ya mwisho kimkoa.
“Wilaya yetu imechafuka kwa sababu ya kutofahamu mtu na uwajibikaji wake kwenye eneo ambalo anasimamia,naomba utengenezwe mfumo wa walimu kutambua wajibu wao kwa watoto na Taifa’’,alisema.
Diwani wa Kata ya Kilagano ametoa rai kwa timu ya ukaguzi wa elimu,kueleza changamoto zipi zinazoikabili sekta ya elimu hadi kutoa matokeo ya chini ya ufaulu.
Akijibu hoja hizo Afisa Elimu Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Songea Tanu Kameka amekiri ufaulu sio wa kuridhisha ambapo ameyataja matokeo ya mwaka 2019 ya darasa la saba Halmashauri ilifaulisha kwa asilimia 71.99 na mwaka 2020 ufaulu ulikuwa wa asilimia 66.66.
Kameka amesema wamefanya tathmini ya elimu kwa kupita kata zote na kuwahusisha wadau wote wa elimu ambapo hivi sasa wanakusudia kufanya ufuatiliaji wa hali ya juu mwaka mzima na kuchukua hatua kwa wasimamizi wa elimu.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Februari 13,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.