MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ameiagiza TAKUKURU kufanya uchunguzi kwa viongozi wa vijiji katika Halmashauri ya Madaba wilayani Songea ambao wanalalamikiwa na wananchi kuuza maelfu ya hekari kinyume cha sheria ya ardhi.
Kanali Thomas ametoa agizo hilo baada ya kusikiliza kero za wananchi wa Kata ya Wino Halmashauri ya Madaba kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Lilondo.
“Yametolewa malalamiko hapa ya baadhi ya Viongozi wa serikali za vijiji kuuza ardhi ya Kijiji bila kufuata utaratibu,nakuagiza Mkuu wa TAKUKURU njoo uchungulie na hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa yeyote atakabainika’’,alisisitiza RC Thomas.
Mkuu wa Mkoa amemuagiza Mkuu wa Wilaya kufuatilia baadhi ya maeneo yaliyovamiwa na watu ambayo yamehifadhiwa katika Halmashauri ya Madaba kwa ajili ya vyanzo vya maji na matumizi ya baadaye ya Kijiji.
Amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Songea kuhakikisha wale wote ambao wameingia kwenye maeneo ambayo yalitengwa na serikali kwa ajili ya hifadhi waondoke na miti yote waliopanda itaifishwe na kuwa mali ya Kijiji.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Kapenjama Ndile ameahidi kutekeleza maagizo ya Mkuu wa Mkoa ambapo amesema viongozi wa vijiji katika Halmashauri ya Madaba, wamepora ardhi kwa udanganyifu kujipatia mamilioni.
Amevitaja vijiji ambavyo uuzaji ardhi unafanyika kwa kasi kinyume cha sheria ya ardhi ni Pamoja na Kijiji cha Mbangamawe ambapo hadi sasa zaidi ya hekari 3000 zimeuzwa na Kijiji cha Ifinga zaidi ya hekari 2000 zimeuzwa huku watu wengine ambao wameuziwa sio raia wa Tanzania.
“Baadhi ya akaunti za viongozi wa vijiji zimebainika wana fedha hadi milioni 40 lakini biashara inayofanyika ni ardhi ya Kijiji,Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kama ulivyoagiza TAKUKURU kwa kweli ardhi ya kijiji inaporwa kwa mikataba ya udanganyifu kwa kiwango kikubwa’’,alisema Ndile.
Amewaomba wananchi wasikubali kudanganywa kuhusu ardhi ambapo amesema vijiji vyote ambavyo viongozi wa vijiji wanalalamikiwa hakuna namna nyingine zaidi ya TAKUKURU kuchunguza na kuwatafuta wote waliohusika.
Ndile amesema kuna baadhi ya vijiji wilayani Songea wananchi wenyewe wameamua kuwatimua viongozi wa vijiji kwa kuuza ardhi kinyume cha sheria na kujipatia mamilioni ya fedha ambapo amesema hivi karibu Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbangamawe ameuza zaidi ya hekari 1000 za Kijiji.
Awali wananchi wa Kata ya Wino wakitoa kero kwa Mkuu Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma waliwataja baadhi ya viongozi wa vijiji kuhusika na migogoro ya ardhi kwa kuuza maelfu ya hekari kwa wawekezaji bila kufuata sheria za ardhi.
Wananchi walidai ardhi ya vijiji inaendelea kuuzwa kwa wawekezaji,na wanapouliza maswali kwa viongozi wao wa vijiji na kata wanaambiwa wanyamaze kwa kuwa wao ni wapiga kelele tu hivyo walimuomba Mkuu wa Mkoa kuwasaidia.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma anaendelea na ziara yake ya kukutana na wananchi kwa lengo la kusikiliza maoni na kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Wino wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma baada ya kueleza kero zao
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.