Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema maji ni raslimali adimu Duniani inayohitaji ulinzi kama zilivyo raslimali nyingine zilizopo kwenye matishio
Kanali Abbas amesema hayo kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea.wakati anafunga mafunzo kwa vyombo vya utoaji huduma ya maji ngazi ya Jamii kwenye mfumo wa kieletroniki wa utoaji ankara za maji na ukusanyaji wa mapato.
Mafunzo hayo yamefanyika kwa siku 13 yakishirikisha washiriki zaidi ya 120 kutoka Wilaya zote tano za Mkoa wa Ruvuma.
“Maji ni moja ya matishio makubwa ya kiusalama Duniani,takwimu zilizopo zinaonesha maji yanaendelea kupungua,watu wameyaona maji kama sehemu muhimu ya bidhaa inayohitaji ulinzi,unaofanana na ulinzi wa raslimali nyingine’’,alisema Kanali Abbas.
Hata hivyo amesema baadhi ya maeneo ikiwemo Tanzania haioni tishio hilo kwa sababu kila eneo unalopita unaona maji yanatiririka ambapo amesema maji yanaweza kuiingiza dunia kwenye migogoro ili watu wasiokuwa na maji waweze kuipata raslimali hiyo.
Amesema licha ya uwepo wa maji katika nchi yetu,mapato yanayotokana na uwepo wa maji yamekuwa ni madogo ukilinganisha raslimali nyingine .
Amesema serikali imeamua kuanzisha mifumo ya udhibiti wa mapato yanayotokana na maji ili kudhibiti mapato ya maji na kuhakikisha huduma za maji zinawafikia wananchi kama serikali ilivyodhamiria kuwatua ndoo kichwani.
Amesisitiza kuwa serikali ya Mkoa hivi sasa ipo makini kubaini matumizi mabaya ya fedha ambazo zitakuwa zinakusanywa kutokana na raslimali ya maji.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Rehema Madenge amewaasa washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha maji yanafika kwenye nyumba za wananchi na fedha inayokusanywa inapelekwa benki.
Amesema kwa kuwa fedha hizo zinakusanywa kupitia mfumo inamaanisha fedha hizo ni za serikali ambazo zina utaratibu wake maalum wa matumizi na kwamba kwenda kinyume na hivyo ni kujitafutia matatizo.
Katibu Tawala huyo amewaomba washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha kuwa fedha itoke kwa utaratibu maalum na kutumika inavyostahili ili kufikia malengo yaliyowekwa badala ya kutumia fedha mbichi.
Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshonga amelitaja lengo mafunzo hayo ni kuhakikisha RUWASA inatekeleza maagizo ya serikali ya kukusanya fedha za serikali kupitia vyombo vya watumiaji maji na kutumika kwa malengo ya serikali.
Lengo la serikali ni kuhakikisha wananchi waishio vijijini wanapata huduma ya maji safi na salama kwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2025.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.