Mkurugenzi wa Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa stakabadhi ghalani nchini Asangye Bangu amesema wamedhamiria kutumia mizani ya kieletroniki katika vyama vyote vya Msingi vya Ushirika (AMCOS)ili kukabiliana na makarani wadanganyifu ambao wamekuwa kero kwa wakulima .
Bangu alikuwa anazungumza na wakulima wa Chama cha Msingi cha Ushirika Mandawa Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi ikiwa ni ziara yake ya kutembelea wakulima wanauza mazao yao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani katika mikoa ya Ruvuma,Lindi,Mtwara na Pwani.
"Tutaweka mizani ya kijiditali katika vyama vyote vya msingi na Ushirika ambayo itasoma namba ambazo mpimaji na mkulima wataona kisha itatoa karatasi iliyochapwa kwenye mashine badala ya kuandikwa kwa mkono",alisisitiza Bangu.
Amesema vipimo hivyo vya kieletroniki ambavyo vitapimwa kwenye AMCOS pia vitaonekana kwenye ghala kuu na Ofisi za Bodi Makao makuu kwa sababu vitakuwa tayari kwenye Mfumo wa kieletroniki.
Amesema kuanza kutumika kwa Mfumo huo kwenye AMCOS zote kutaondoa kwa asilimia zaidi ya 70 malalamiko kwa wakulima wanauza mazao yao kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani.
Mkurugenzi huyo wa Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa stakabadhi ghalani ameitaja hatua nyingine ambayo wanatarajia kuichukua ni kuratibu wasafirisha wa mazao ya wakulima kutoka kwenye maghala ya kwenye AMCOS na kupeleka kwenye maghala makuu ya vyama vya Ushirika.
Amesema watahakikisha magari yote yamesajiriwa na watachukua hatua kwa dereva au mmiliki wa gari ambaye atabainika kuhujumu mazao ya wakulima.
Amesema uchunguzi walioufanya wamebaini malalamiko mengi yanatokea kabla mzigo haujafika kwenye ghala kuu .
"Lengo letu tunataka kila mtu aogope mali ya mkulima aone kama amekutana na moto,sipo tayari kuona wakulima wanaendelea kulalamika na kuona kama vile Mfumo wa stakabadhi ghalani haufai wakati wakulima wengi wanaupenda ",alisisitiza.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Hassa Ngoma akizungumzia Mfumo wa stakabadhi ghalani amesema mfumo huo unawasaidia wakulima wengi isipokuwa changamoto zilizopo wakati wa utekelezaji wa Mfumo huo zinatakiwa kupatiwa ufumbuzi.
Amesema wakulima hawana tatizo na Mfumo isipokuwa kinachotakiwa ni maboresha ili kuleta tija zaidi.
Ameunga mkono matumizi ya mizani ya kieletroniki ambayo amesema itamaliza udanganyifu wa baadhi ya makarani ambao sio waaminifu ambao wamekuwa wanadaiwa kuwapunja wakulima.
Said Mohamed Kassim Mkulima wa kijiji cha Mandawa Wilaya ya Ruangwa amesema kuna changamoto kubwa kwenye upimaji mizani ya kuandikwa stakabadhi kwa mkono ambapo kumekuwa na tofauti ya uzito hali ambayo inaleta shida kwenye malipo.
Ameunga mkono wazo la kufunga mizani za kieletroniki kwenye AMCOS ambapo amesema zitamaliza changamoto hiyo.
Zuhura Ally Juma Mkulima wa kijiji cha Mandawa amedai mizani inayotumika kupima mazao yao hawana imani nayo wanaomba kubadilishiwa kwa sababu imekuwa inatoa vipimo tofauti na kuleta manung'uniko makubwa kwa wakulima wa korosho.
Zao la korosho ambalo litajwa kuwa dhahabu ya kijani ni zao la kwanza la kimkakati linalochangia maendeleo ya uchumi kwa wananchi na serikali kwa ujumla.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Julai 23,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.