Makumbusho ya mashujaa wa Vita ya Majimaji Songea, mkoani Ruvuma, yanatarajiwa kubadilika sura, kutoka sanamu za kawaida kwenda sura halisi za mashujaa walioshiriki vita hiyo, hatua inayolenga kuwakumbuka kwa uhalisia zaidi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Makumbusho na Mali Kale Makumbusho ya Taifa, Adelaide Sallema, wakati wa kikao chake na wajumbe wa Baraza la Makumbusho na Machief wa Songea.
Alifafanua kuwa lengo ni kuutambulisha mradi wa uumbaji upya wa sanamu 12 za mashujaa wa Majimaji, ili zifanane na sura halisi za wahusika.
Sallema alibainisha kwamba mradi huo wa uboreshaji una lengo la kuhifadhi historia ya Vita ya Majimaji kwa uhalisi, kuleta mvuto wa kipekee wa utalii wa kihistoria, na kuimarisha urithi wa kitamaduni wa Taifa.
Aliongeza kwamba mabadiliko haya yatawasaidia wageni, wanafunzi, na jamii ya Kitanzania kuijua vyema historia ya mashujaa wa Majimaji.
Kikao hicho, kilichofanyika viwanja vya Makumbusho ya Majimaji Songea, kilihudhuriwa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akiwemo Mhadhiri na Mkuu wa Makumbusho Kanda ya Kusini Nyanda za Juu, Frola Vicent.
Wataalamu hao walishirikiana kutoa maoni ya jinsi mradi huo utakavyotekelezwa.
Maboresho haya yanatarajiwa kuleta sura mpya ya Makumbusho ya Majimaji Songea, yakiboresha mvuto wa utalii wa kihistoria, kuhamasisha umma kuuthamini urithi wa taifa, na kutoa fursa kwa vizazi vijavyo kujifunza historia ya mashujaa wa Majimaji kupitia taswira halisi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: KERO PIGA 0800110174
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.