Kijiji cha Mbati kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kimebarikiwa kuwa na msitu wenye magogo yaliyogeuka mawe hali inayosababisha kutembelewa na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
Mratibu wa Utalii Kanda ya Kusini ambaye pia ni Afisa Msaidizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Tunduru Debora Mwakanosya amesema miti inayogeuka mawe (Miti mawe) ni jamii ya miti ya mitetereka ambayo duniani inapatikana nchi mbili ambazo ni Marekani na Tanzania.
“Kwa Tanzania miti mawe inapatikana Mkoa wa Ruvuma katika kijiji cha Mbati wilaya ya Tunduru,pia miti hiyo inapatikana katika Wilaya ya Namtumbo eneo la Likuyu Hifadhi ya Taifa ya Nyerere na katika pori la Akiba la Liparamba wilaya ya Nyasa’’,alisema.
Amesema mti huo ukiuona juu kabla ya kugeuka jiwe unakuwa ni mti wa kawaida na kwamba mti huo unageuka jiwe kutokana na mfumo wa asili ambao Mungu ameutengeneza kwa kuwa mti huo unageuka jiwe zito kabisa.
Amesema kivutio hicho cha miti mawe kinaufanya utalii wa Mkoa wa Ruvuma kuwa ni wa kipekee na tofauti kabisa na kwamba aina hiyo ya miti ina uwezo wa kudumu zaidi ya miaka 120.
Hata hivyo Mtaalamu huyo wa miti amesema miti hiyo ipo katika hatari kubwa ya kutoweka kutokana na watu wengi kuikata kwa matumizi mbalimbali,ambapo amesisitiza miti hiyo inatakiwa kuhifadhiwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Naye Sandali Mtenje Mzee maarufu katika kijiji cha Mbati chenye msitu wenye magogo yaliyogeuka mawe,amesema aliona vipande vya mti uliogeuka mawe tangu mwaka 1983 na kwamba miaka hiyo vipande hivyo vya magogo vilikuwa katika hatua za awali za kugeuka mawe.
Sandali anasema miaka tisini waliona wageni wengi wanatembelea mara kwa mara msitu wa kijiji hicho wakiwemo raia wa kigeni ambao walifika kuona miti hiyo ikiwa imegeuka mawe.
“Baada ya muda tukagundua wazungu wanafika hapa tena bila hata kuona viongozi wa kijiji wanapandua magamba ya miti hiyo na wengine wanachukua vipande vya miti iliyogeuka mawe na kuondoka navyo’’,alisema Sandali.
Utafiti uliofanywa katika pori la akiba Selous ambalo sasa ni hifadhi ya Taifa ya Nyerere na wataalam kutoka nje ya nchi kwa kushirikiana na wataalam wa Wizara ya Maliasili na Utalii umebaini kupatikana zaidi ya aina(species) 2100 za mimea zilizotambuliwa na wanasayansi ikiwemo aina 600 za miti ambayo haipatikani sehemu nyingine duniani.
Mkurugenzi Mstaafu wa Uhifadhi ambaye pia amewahi kuwa Mkuu wa Chuo cha Wanyamapori Likuyuseka Namtumbo Ngwatura Ndunguru anaitaja Moja ya jamii ya miti ambayo haijafahamika na kutangazwa ipasavyo kuwa ni magogo ya miti iliyogeuka mawe jamii ya miti ya mitetereka ambayo kitaalam inaitwa fossilized tree trucks .
Amesema masalio ya magogo hayo bado yanaonekana katika baadhi ya maeneo ya ndani hifadhi ya Selous(Hifadhi ya Taifa ya Nyerere) na katika vijiji vya Mpurakacheche na Mbarang’andu Wilaya ya Namtumbo Mkoa wa Ruvuma.
Ngwatura anasisitiza kuwa miti mawe hiyo ikitangazwa kwenye vyombo vya habari,mamia ya watalii wanaweza kufika katika Mkoa wa Ruvuma na kuona kivutio hicho kipya na cha kipekee hivyo kuingiza mapato na fedha za kigeni ambazo zitasaidia kuinua uchumi wa Taifa.
Kwa upande wake Afisa Utalii wa Pori la akiba Liparamba wilayani Nyasa Maajabu Mbogo amesema miti mawe inapatikana kwa wingi katika eneo la Nakatuta ndani ya hifadhi hiyo.
Kwa mujibu wa Mhifadhi huyo,maeneo yote ambayo miti imegeuka mawe hayakaliwi na watu wengi wala hakuna mtu anayeingia ndani ya eneo hilo hali iliyosababisha maeneo hayo kubakia katika hali yake ya asili ya kijiolojia ya kutoharibiwa kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Desemba 7,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.