MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amezindua mpango wa kugawa hati miliki za kimila zaidi ya 1000 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma.
Mndeme amezindua hati hizo kati ya hatimiliki zaidi ya 26,000 zilizotengenezwa na Halmashauri hiyo kwa ajili ya kugawawiwa vijiji 86 katika soko la Mnadani kijiji cha Nyoni.
,Mndeme amesema Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli ametimiza ahadi aliyotoa kwa watanzania ya kuhakikisha migogoro ya ardhi inamalizika kwa kupanga kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi kwa kila mwananchi.
Mndeme amevitaja vijiji vitano vya Kata ya Nyoni ni kati ya vijiji 86 ambavyo vimenufaika na mpango wa hati miliki za kimila katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga . Katika hafla hiyo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amewakabidhi hati wakulima 20 wa Kata ya Nyoni kwa niaba ya kata 24 zilizopo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
“Naomba Kuanzia sasa watu wa Benki mzitambue nyaraka hizi za hati miliki za kimila kuwa ni halali na wanaweza kuzitumia sehemu yeyote na vyombo vya kisheria kwa sababu mashamba haya yanakwenda kutambulika rasimi”. Amesema Mndeme.Mndeme pia amewapongeza Mkuu wa Wilaya ya Mbinga na Mkurugenzi wa Halmashauri kwa kufanikisha zoezi hilo ambalo limegharimu zaidi ya shilingi bilioni moja katika upimaji wa mashamba ambao umehusisha vijiji 86 vyenye ekari takiribani 59,000.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye amesema atahakikisha kila kipande ambacho kipo katika halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kinapimwa ambapo ametoa rai kwa wananchi ambao hawajapimiwa kuondoa hofu kuhusu zoezi hilo ambalo ni endelevu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Mbinga Juma Mnwele, amesema ekari 70,000 ya mashamba ya mazao ya kudumu ambayo ni sawa na mashamba 26,247 yametambuliwa na kupimwa.Hata hivyo Mnwele amesema Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga imeweza kutengeneza hatimiliki za kimila 26,247 katika vijiji 86 zilizogharimu zaidi ya shilingi bilioni moja na vijiji hivyo ni kati ya vijiji 117 vya Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga.
Naye mkulima wa kijiji cha Nyoni Ponziana Nzuyu amemshukuru Rais Dkt.John Magufuli kwa kuwaunga mkono wakulima ambapo ametoa rai kwa wataalam kuendelea kuwaelimisha wananchi faida za hatimiliki.
Imeandaliwa na Farida Mussa
Kutoka Ofisi ya Habari Mkoa wa Ruvuma
Oktoba 10,2029
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.