MIKOA mitano ya Mbeya,Iringa,Ruvuma,Songwe na Njombe inapata mafunzo ya siku tano ya kikao kazi cha zoezi la kuingiza mezani kuhusu udhibiti wa homa ya nguruwe Nyanda za Juu kusini.
Mafunzo hayo ambayo yanafanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Mkapa mjini Mbeya,yanaendeshwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Kurugenzi ya Huduma za Mifugo kwa ushirikiano na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho,Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo na Uvuvi Wizara ya Mifugo na Uvuvi Profesa Henzron Nonga amewataja wadau wanaohusika katika kikao hicho kuwa ni wafugaji,wafanyabiashara,wachinjaji,Chama cha wafugaji wa nguruwe,polisi,wanahabari na washirika wa maendeleo.
Kwa mujibu wa Profesa Nonga,Tanzania ina nguruwe wanaofikia milioni 2.14 na kwamba ufugaji wa nguruwe umekuwa unakabiliwa na changamoto nyingi,kubwa zaidi ikiwa ni ugonjwa wa homa ya nguruwe(African Swine fever).
“Ugonjwa wa homa ya nguruwe ni tatizo kubwa katika utekelezaji wa tasnia ya nguruwe kwa sababu ugonjwa unaua nguruwe wengi kwa wakati mmoja,pia ugonjwa huo hauna chanjo wala tiba’’,alisisitiza Profesa Nonga.
Tafiti zinaonesha kuwa mlipuko wa ugonjwa huo,unaweza kusababisha hasara ya mpaka shilingi 2,094,922,800 kwa mwaka na kwamba kutokana na hali hiyo,Profesa Nonga amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imelazimika kuwaleta wadau wa tasnia ya nguruwe pamoja ili kubadilishana uzoefu wa namna ya kudhibiti homa ya nguruwe ambayo inaua kwa asilimia 100.
Kwa upande wake mgeni rasmi katika mafunzo hayo Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Said Juma Madito amesema Wizara imeamua kuwakutanisha wadau wote wa nguruwe ili kila mmoja afahamu namna bora ya kukabiliana na homa ya nguruwe ambayo imeathiri kwa kiwango kikubwa nguruwe waliopo katika Nyanda za juu Kusini.
Amesema wadau wote wa nguruwe wakizungumza lugha moja,ugonjwa huo unaweza kudhibitiwa ambapo amesema katika Mkoa wa Mbeya pekee kuna nguruwe zaidi ya laki mbili hivyo isipowekwa mikakati na mbinu za pamoja katika kukabiliana na homa hiyo inaweza kuwa janga kubwa kwa wafugaji.
“Wadau tunatakiwa kuelewa kuwa ufugaji wa nguruwe ni uchumi mkubwa baada ya ng’ombe, kwa sababu sisi Nyanda za Juu kusini katika chakula na mifugo tunalisha mikoa mingine na nchi jirani’’,alisisitiza Madito.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Profesa Gerald Misinzo akitoa mada ya homa ya nguruwe amesema homa hiyo iligundulika mwaka 1910 ambapo hivi sasa imeathiri dunia nzima ikiwemo Tanzania na kwamba tangu ulipolipuka ugonjwa huo mwaka 2010 umesambaa maeneo mengi na kusababisha hasara kubwa.
Ameutaja ugonjwa wa homa ya nguruwe kuwa unasambaa kupitia kupe laini kwa kunyonya damu ya nguruwe asiye na ugonjwa na kwamba ugonjwa uenea kwa njia ya kugusana na majimaji au damu ya nguruwe mgonjwa.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wa Nguruwe Tanzania(TAPIFA) Doreen Maro amesema chama hicho kimefanikiwa kuingiza mbegu bora za kisasa za nguruwe 280,000 ambazo zimesambazwa nchi nzima ili kuhakikisha wafugaji wanazalisha nguruwe bora,wenye uzito mkubwa ili kuongeza kipato kwa mfugaji.
Profesa Folorunso Fasina ni Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa FAO amesema ufugaji wa nguruwe ukifanyika kwa tija na ufanisi unaweza kuleta faida na kuingiza kipato kikubwa kwa mfugaji kwa sababu maingizo yake kwa mwaka ni zaidi ya shilingi bilioni mbili.
Hata hivyo amesema homa ya nguruwe ni changamoto kubwa ambayo inaweza kuleta umaskini mkubwa kwa mfugaji kwa sababu ugonjwa unaua karibu nguruwe wote walioathirika na homa ya virusi vya nguruwe.
Ametoa rai kwa wadau wa nguruwe kushirikiana kwa kutoa elimu hasa kuwatumia wanahabari ambao wanaweza kufikisha elimu ya kukabiliana na homa ya nguruwe kwa watu wengi ndani ya muda mfupi.
Tushirikiane,tuunganishe nguvu kwa pamoja katika kuutokomeza ugonjwa wa homa ya nguruwe ambayo inaweza kubakia historia endapo kila mdau wa nguruwe atatimiza wajibu wake.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Agosti 12,2020
Mbeya
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.