SERIKALI imetoa Sh.milioni 450 kwa Halmashauri ya wilaya Songea mkoani Ruvuma,ili kujenga vyumba kumi vya madarasa na shule moja ya msingi ikiwa ni maandalizi ya kupokea wanafunzi watakaochaguliwa kuanza kidato cha kwanza na wanaotarajia kuanza elimu ya msingi mwezi Januari 2023.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Neema Maghembe,wakati akitoa taarifa ya maandalizi ya ujenzi wa madarasa hayo ofisini kwake kijiji cha Lundusi kata ya Maposeni km 28 kutoka Songea mjini.
Maghembe alieleza kuwa,kati ya fedha hizo Sh.milioni 200 zitatumika kujenga vyumba kumi vya madarasa kwenye shule za sekondari zilizoanishwa kuwa na upungufu,ambapo Halmashauri imeshaanza taratibu za awali za ujenzi madarasa hayo.
Aidha alisema,Sh.milioni 250 zitatumika kujenga shule ya msingi katika kitongoji cha Lizaboni kata ya Muhukuru mpakani mwa Tanzania na Msumbiji ambako katika eneo hilo ,watoto wanalazimika kutembea umbali mrefu kwenda shule mama ya Matama.
Alisema,Serikali ya awamu ya sita imetoa fedha hizo ikiwa ni mkakati wa kuimarisha na kuboresha sekta ya elimu hususani ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa, kwenye maeneo ambayo watoto wanalazimika kwenda vijiji vingine mbali na makazi yao kufuata shule.
Alisema,fedha hizo tayari zipo kwenye akaunti ya serikali ya kijiji ambapo wazazi na jamii ya eneo hilo wameshaanza kazi ya ujenzi ili shule zitakapofunguliwa mwezi Januri mwakani watoto wenye sifa ya kuanza elimu ya awali na msingi wayatumie madarasa hayo.
Maghembe,ameishukuru serikali ya awamu ya sita kutoa fedha hizo ambazo zinakwenda kumaliza tatizo la vyumba vya madarasa kwa wanafunzi wanaotarajiwa kuingia kidato cha kwanza na shule za msingi mwakani.Amewataka watendaji na watumishi walioteuliwa kwenda kusimamia ujenzi wa madarasa hayo, kuhakikisha wanashiriki na kusimamia miradi hiyo kikamilifu ili kupata thamani halisi ya fedha na kujiepusha na wizi na aina yoyote ya ubadhirifu.
Pia alisema,hadi sasa wamepokea jumla ya walimu wa ajira mpya 44 wa shule za msingi na sekondari na walimu hao wameshapangiwa kwenye vituo vyao vya kazi na wanaendelea kufanya kazi ya kuwapatia watoto elimu bora.
Katika hatua nyingine Maghembe alisema,Halmashauri kupitia mapato yake ya ndani kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 inaratajia kujenga nyumba za walimu sambamba na kuongeza matundu ya vyoo kwa kila shule ya msingi.
Alisema,hatua hiyo ni mkakati wa Halmashauri hiyo ya kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu wanaofanya kazi kwenye mazingira magumu hasa katika shule za msingi shikizi za Lihuhu,Lunyele,Jenista Mhagama,Lizaboni na maeneo mengine.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.