Mkoa wa Ruvuma umeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuboresha miundombinu ya elimu kupitia Programu ya BOOST, mradi mkubwa wa ujenzi wa shule mpya na ukarabati wa miundombinu ya shule za msingi.
Jumla ya shule mpya za msingi 12 zimejengwa, pamoja na miundombinu mbalimbali katika shule za msingi 44, kwa gharama ya shilingi bilioni 7.29.
Ujenzi wa shule zote umefanikiwa kwa asilimia mia moja, na tayari shule hizo zimeanza kutumika, hatua inayotarajiwa kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto wa mkoa huu.
Mbali na juhudi hizo, Mkoa wa Ruvuma pia umeendelea kupokea fedha kwa ajili ya miradi mingine muhimu ya elimu inayolenga kuinua viwango vya elimu ya sekondari kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP).
Katika kipindi cha Januari 2021 hadi Desemba 2024, jumla ya shilingi bilioni 3.43 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 20, mabweni 22, na matundu ya vyoo 82.
Miradi hii inalenga kuboresha shule zilizopandishwa hadhi kuwa na madarasa ya kidato cha tano na sita, pamoja na shule zenye idadi kubwa ya wanafunzi, na inatekelezwa katika halmashauri za Namtumbo, Songea Vijijini, Songea Manispaa, na Tunduru.
Katika kuhakikisha walimu wanapata makazi bora, Mkoa wa Ruvuma umepewa shilingi milioni 950 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 10 za walimu, kila moja ikiwa na uwezo wa kuchukua familia mbili (2 in 1).
Ujenzi huu unatekelezwa katika halmashauri zote nane za mkoa, hatua inayotarajiwa kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu na kuongeza ufanisi katika ufundishaji.
Mkoa pia umepokea zaidi ya shilingi bilioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya 9 za sekondari kupitia awamu ya tatu ya Mradi wa SEQUIP.
Shule hizi zitajengwa katika majimbo yote ya uchaguzi ndani ya Mkoa wa Ruvuma, ikiwa ni juhudi za kuimarisha upatikanaji wa elimu ya sekondari kwa vijana wa mkoa huu.
Miradi hii inadhihirisha dhamira ya serikali ya kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bora kwa kuweka mazingira mazuri ya kujifunzia.
Mafanikio haya ni ushahidi wa uwekezaji wa serikali katika sekta ya elimu, hatua inayosaidia kujenga jamii iliyoelimika na yenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.