Mji wa Peramiho uliopo Wilaya ya Songea Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa miji ya zamani yenye historia ya kipekee katika ukanda ya kusini.
Mji wa huo unafahamika zaidi nje ya nchi pengine kuliko miji mingine iliyopo kusini mwa Tanzania kutokana na mji huo kuwa na historia ya namna yake kipekee ikiunganisha Tanzania na mataifa ya Ulaya.
Historia ya mji wa Peramiho uliopo kilometa 24 tu kutoka makao makuu ya mkoa wa Ruvuma Songea inaunganishwa na wabenediktini wa kanisa katoliki kutoka St.Otilia nchini Ujerumani, ambao waliamua kuweka makao makuu yao katika Abasia ya Peramiho.
Wabeneditine hao waliingia kwa mara ya kwanza katika mji huo mkongwe mwaka 1898 wakiongozwa na Kasian Spiss. Tangu wakati huo wabenediktine hao wamekuwa wakifanya mambo yanayoutangaza mji huo hali iliyosababisha kuutambua mji wa Peramiho kuwa ni mji unaokidhi vigezo kuwa mji wenye utalii wa kiutamaduni.
Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa Philipo Maligisu anasema wabenediktine wa Abasia ya Peramiho wametengeneza historia ya kipekee na kuvutia katika nchi ya Tanzania ambao wameacha historia katika mji wa Peramiho na taifa kwa ujumla hasa walipojikita katika suala zima la elimu na kuamua kuwekeza katika elimu kwa zaidi ya miaka 100 iliyopita.
Historia inaonesha kuwa walipoingia kwa mara ya kwanza wabenediktine hao kwa kutambua umuhimu wa elimu waliamua kuanzisha madarasa kwa kufundisha walimu na kufundisha wanafunzi hivyo kufundisha elimu zote mbili yaani elimu ya kiroho na elimu dunia
Kwa msingi huo eneo la Peramiho katika historia ya Tanzania ina historia ya kipekee kwa zaidi ya miaka 100 hivyo kuna ushahidi ambao unaonesha wabenediktine walidhamiria kufanya mambo ya msingi katika mji wa Peramiho na taifa kwa ujumla.
Utafiti uliofanywa katika mji wa Peramiho unaonesha kuwa wabenediktine hao walizindua rasmi mji huo Julai 31,1898 na tangu hapo waliendelea na shughuli zao wakiwa na mahusiano mazuri wakati huo na utawala wa machifu katika eneo hilo.
Hata hivyo mahusiano hayo mazuri baina ya wabenedikitine hao kutoka nchini Ujerumani na machifu ulikuja kuharibika wakati wa vita ya Majimaji ambayo vilianza mwaka 1905 na kumalizika mwaka 1907 na kusababisha padre Fransis Scuss wa Abasia hiyo kuuawa Septemba 9 1905.
Baada ya kumalizika vita hiyo, ilijitengeneza tena historia mpya ya kanisa la Abasia ya Peramiho hivyo kulichukulia eneo hilo kama eneo la kipekee kwa kuzingatia misingi ya sheria ya Tanzania namba 10 ya mwaka 1964 na maboresho yake namba 22 ya mwaka 1979 ambayo inayatambua maeneo yote ya kihistoria kulingana na umuhimu wake katika jamii.
Wananchi wa Ujerumani wanaijua Peramiho pengine kuliko hata sisi watanzania,ndiyo maana kizazi na kizazi wanasafiri kwa gharama kubwa hadi katika mji huo ili kufanya utalii wa kiutamaduni kwa kutembelea katika maeneo mbalimbali ya kihistoria ili kujifunza mambo mbalimbali.
Sera ya Taifa ya utamaduni ya mwaka 1997 ina tamka bayana kuwa eneo lolote la kihistoria linapokuwa limetimiza miaka 100 tayari moja kwa moja linaingia katika urithi wa utamaduni wa taifa.
Kutokana na hali hiyo ukiangalia mji huo wa Peramiho tayari umekidhi vigezo na maeneo yake yote ya kihistoria kuingia katika urithi wa utamaduni wa taifa kwa ajili ya kujifunza elimu na utalii
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.