MKOA wa Ruvuma umeridhia kupandisha hadi Hifadhi mbili za misitu kuwa mapori ya akiba (Game Reserve) kwa lengo la kuendeleza sekta ya maliasili na utalii.
Afisa Maliasili Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Africanus Challe ameyataja mapori hayo kuwa ni Gesimasowa lililopo Madaba lenye ukubwa wa kilometa za mraba 764 na pori la Litumbandyosi lililopo Mbinga lenye ukubwa wa kilometa za mraba 494.
Amayataja mapori hayo kuwa ni Sehemu ekolojia ya Selous Niassa na kwamba mpaka sasa bado mapori hayo hayajapata Tangazo la Serikali la kuwa na mapori ya akiba rasmi.
Kwa mujibu wa Afisa Maliasili huyo,Mkoa una mpango wa kuanzisha mashamba ya Wanyamapori (Wildlife Farms) katika Kisiwa cha Lundo ziwa Nyasa wilaya ya Nyasa pamoja na Chuo cha Maliasili cha Likuyusekamaganga wilayani Namtumbo ili wananchi waweze kujifunze kutoka mashamba ya wanyamapori ya serikali ili wao waweze kuanzisha mashamba binafsi ya wanyamapori.
Hata hivyo Challe amesema Mkoa wa Ruvuma unakabiliwa na changamoto kubwa ya Wanyamapori waharibifu hasa Tembo hivyo kuharibu mali na kuhatarisha maisha.
“kwa kipindi cha Miaka mitano iliyopita matukio ya Wanyamapori Waharibifu na wakali imekuwa ikiongezeka katika wilaya za Tunduru na Namtumbo hivyo kusababisha ongezeko la fedha za kifuta jasho na kifuta machozi zinazolipwa kwa jamii zilizoathirika’’,alisema.
Kulingana na Afisa Maliasili huyo mwaka 2019/2020 jumla ya wananchi 1625 waliathirika na wanyamapori wakali na waharibifu dhidi ya mali na maisha ya binadamu.
Ameongeza kuwa katika kipindi hicho jumla ya ekari 2879.33 ziliharibiwa, wananchi wawili walijeruhiwa na wananchi wanne waliuwawa na wanyamapori.
Challe amebainisha zaidi kuwa mwaka 2020/2021 jumla ya watu 435 waliathirika na wanyamapori na jumla ya ekari 2562.83 ziliharibiwa, watu saba waliowawa na watu sita kujeruhiwa.
Hata hivyo amesema malipo ya fedha ya kifuta jasho na kifuta machozi yamefanyika katika Wilaya ya Tunduru ambapo takribani shilingi milioni 270,650,000 zimelipwa kwa waathirika katika kipindi cha mwaka 2020/2021 na mwaka 2019/2020.
Amesema licha ya jitihada zinazochukuliwa na Mkoa kukabiliana na wanyamapori waharibifu,Mkoa umependekeza tembo waweze kurejeshwa kwenye makazi yao.
Amezitaja hatua nyingine za kukabiliana na wanyamapori waharibifu kuwa ni Wizara ya Maliasili na Utalii,TAWA,TANAPA kwa kushirikiana na Halmashauri kuanzisha vituo vya askari vya kudumu vya kudhibiti wanyamapori waharibifu kwenye maeneo korofi na kuziwezesha Halmashauri vitendea kazi kama mahema, gari na mafuta, Silaha, risasi na vilipuzi kwa ajili ya kupambana na wanyamapori waharibifu hususani tembo.
Amezitaja hatua nyingine kuwa ni Wizara kutenga bajeti au fedha kwa ajili ya kudhibiti wanyamapori waharibifu kwenye Wilaya zenye changamoto hasa Tunduru na Namtumbo.
Hatua nyingine amezitaja kuwa ni Wizara ya Maliasili na Utalii kutumia ndege zisizo na rubani (drone) na helcopter kuwaondoa Tembo katika maeneo jirani na makazi ikiwemo hifadhi ya msitu wa Mlima Kipiki wilayani Namtumbo.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Januari 18,2023
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.