MKOA wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa michache nchini ambayo imebarikiwa na Mwenyezi Mungu kuwa na vivutio vya aina zote za utalii,ambazo ni utalii wa ikolojia na utamaduni.
Mkoa wa Ruvuma una mapori manne ya wanyamapori ambayo ni sehemu ya mfumo wa Selous.Mapori hayo ni Selous lenye ukubwa wa kilometa za mraba 50,000,Pori la Liparamba lenye kilometa za mraba 571,Gesimasoa lenye kilometa za mraba 764 na Litumbandyosi lenye kilometa za mraba 464.
Hata hivyo utafiti umebaini bado kuna vivutio vingi ambavyo havijaibuliwa na kutambuliwa ili kutoa fursa za uwekezaji kwa watalii toka ndani na nje ya nchi.
Afisa Maliasili wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anasema vivutio hivyo vikiendelezwa vinaweza kuchangia pato la Taifa na kuinua uchumi wa wananchi na kwamba kinachotakiwa ni kuboresha miundombinu ya barabara na hoteli za kitalii ili kuvutia watalii kuvifikia vivutio hivyo.
Utafiti umebaini karibu kila wilaya iliyopo katika mkoa wa Ruvuma ina vivutio mbalimbali vya utalii vinavyoweza kufungua milango ya utalii katika wilaya husika na kutoa ajira kwa vijana kupitia sekta hiyo adimu hapa nchini na duniani kote.
Hebu tuone baadhi ya vivutio vya utalii ambavyo vipo kila wilaya mkoani Ruvuma,tukianza na wilaya ya Nyasa mjini Mbambabay kuna fukwe,visiwa,samaki wa mapambo,hifadhi ya Ndengere, utalii wa michezo ya majini na majengo ya malikale ya makanisa ya Lituhi na Lundu
Eneo la Liuli wilayani Nyasa kuna vivutio vya Jiwe la kihistoria la Pomonda,fukwe,samaki wa mapambo,historia ya kanisa la Anglikana Tanzania,michezo ya majini,ngoma za asili za kioda na mganda.
Katika eneo la Lundu wilayani humo,kuna vivutio vya jiwe la Chingata,fukwe za samaki wa mapambo,hifadhi ya misitu ya asili ya Lilengalinga,majengo ya historia,michezo ya majini na ngoma za asili.
Wilaya ya Mbinga,nayo imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya utalii vikiwemo bustani ya wanyama ya Lugari,jiwe la maajabu la Mbuji,kilimo cha Ngoro na pori la Liparamba ambalo linafaa kwa utalii wa picha,utafiti wa mimea na utalii wa uwindaji.
Maeneo mengine ya utalii katika wilaya ya Mbinga ni Hifadhi ya Litumbandyosi ambayo inafaa kwa utalii wa picha,utafiti wa malikale na utalii wa kuwinda na Mapango ya wamatengo yaliopo Litembo.
Tukiangalia katika wilaya ya Songea,kuna Hifadhi ya Gesimasowa ambayo inafaa kwa utafiti wa aina mbalimbali,kuwinda na utafiti wa malikale,Hifadhi ya asili ya Luhira,Hifadhi ya Misitu ya milima ya Matogoro,Makumbusho ya Taifa ya Majimaji,Makumbusho ya Mzee Kawawa na Pango la Mlima Chandamali ambalo lilikuwa maficho ya Nduna Songea Mbano wakati wa Vita ya Majimaji.
Vivutio vingine vilivyopo katika wilaya ya Songea ni Bwawa la Tulila,maporomoko ya Mto Ruvuma,majengo na majumba ya kihistoria likiwemo kanisa kongwe la Peramiho.
Vivutio vya utalii vilivyopo katika wilaya ya Tunduru ni Pori la Selous kanda ya Kalulu linalofaa kwa utalii wa uwindaji,Hifadhi ya asili ya Mwambesi inayofaa kwa utalii wa picha na utafiti,eneo la utalii wa mambokale la Masonya na njia ya kusafirishia watumwa ya Mbatamila hadi Masonya ambako ilikuwa kambi ya wakimbizi na ofisi za vyama vya FRELIMO toka Msumbiji.
Katika wilaya ya Tunduru kuna njia ya watumwa ya Kusini iliyokuwa inapitisha watumwa toka Msumbiji kupitia mkoa wa Ruvuma hadi Mikindani mkoani Mtwara ambako kulikuwa na soko la watumwa.
Katika wilaya ya Namtumbo kuna vivutio vya utalii ambavyo ni Pori la Akiba la Selous,Kanda ya Likuyuseka ambayo inafaa kwa uwindaji wa utalii na utalii wa picha na Mji mdogo wa Lusewa katika maeneo ya Kimbanda na Kisungule ambako kunafaa kwa utalii wa kuwinda na picha.
Hata hivyo Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma anasema ili vivutio hivyo viweze kufikika na kuwahudumia watalii kwa uhakika inatakiwa kuboresha miundombinu yake ili kuvutia wawekezaji na watalii.
Anashauri wadau wote katika maeneo husika zikiwemo Halmashauri,Wakala wa Barabara Mkoa TANROAD,Wakala wa Barabara wilaya TARURA,wamiliki wa hoteli, wafanyabiashara na wananchi wote kushirikiana ili kuongeza watalii watakaopenda kuwekeza na kutalii katika mkoa wa Ruvuma.
Challe anautaja mpango mkakati wa kukuza uchumi katika utalii mkoani Ruvuma kuwa ni kuwepo kwa njia kuu nne za kuingia watalii ambazo ni Madaba,Mkenda,Mbambabay na Tunduru.
“Watalii hawa huingia kutoka ndani ya nchi kupitia hifadhi ya Kitulo,Ruaha,Mikumi na Selous au toka nje ya nchi kama Msumbiji,Malawi,Zambia,Zimbabwe na Afrika ya Kusini nchi ambayo inaoongoza kwa utalii barani Afrika’’,anasisitiza Challe.
Hata hivyo Challe anasema watalii wanaingia katika Mkoa wa Ruvuma kwa kiasi kidogo,kwa sababu ya kukosa mawasiliano na vituo vya taarifa za utalii vya mikoa jirani na nchi za jirani.
Anazitaja njia kuu mbili za kupita watalii toka nje ya mkoa wa Ruvuma hadi kwenye vituo vya utalii kuwa ni Njia ya Magharibi ambayo inapitia Mkenda-Liparamba-Tingi-Mbambabay-Liuli-Lundu-Lituhi-Litumbandyosi hadi Madaba.
Njia ya Mashariki anaitaja kuwa inaanzia Songea-Namtumbo-Likuyusekamaganga-Kalulu-Tunduru-Likumbule-Nalasi-Magazini-Lusewa hadi Songea na kwamba mkakati wa kukuza utalii katika mkoa wa Ruvuma unaonesha maeneo mapya muhimu ya uwekezaji wa hoteli za kitalii au camp site.
Afisa huyo wa Maliasili na Utalii anayataja maeneo hayo kuwa ni fukwe kando kando mwa ziwa Nyasa yakiwemo Mtupale hadi Lituhi,kijiji cha Chimate,Liuli,Lundu na Lituhi.
Maeneo mengine ni kando kando ya hifadhi yakiwemo kijiji cha Liparamba,Litumbandyosi,Kazamoyo,Muhuwesi,Ngapa,Likuyusekamaganga na Madaba.
Maeneo mengine ya uwekezaji yaliopo karibu na miji ya vivuko mpakani mwa Tanzania na Msumbiji anayataja kuwa ni Mkenda, Lukumbule na Magazini na makao makuu ya wilaya za Songea, Mbinga,Tunduru,Namtumbo na Mbambabay.
Hata hivyo Challe anasema sekta ya utalii katika Ukanda wa mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi inafanana kiikolojia na mikoa ya kaskazini ya nchi za Msumbiji,Afrika ya Kusini na Malawi.
Challe anabainisha kuwa licha ya mikoa hiyo kuwa na mahusiano mazuri ya kihistoria katika biashara ya utumwa ya kusini,vita ya wangoni na vita ya wapigania uhuru,bado aina hiyo ya utalii haijaendelezwa na kutangazwa.
Anasisitiza kuwa utalii huu wa kihistoria, kiutamaduni, kishujaa, utalii wa wanyamapori na mimea hauna uhusiano mzuri na haujatangazwa katika nchi hizo za kusini kwa kwamba baadhi ya maeneo hayana miundombinu ya uhakika kama barabara, madaraja,viwanja vya ndege na hoteli za kitalii.
Changamoto nyingine anaitaja kuwa ni uhaba mkubwa wa wafanyakazi wataalam,hakuna kampuni au Taasisi za kitalii(Tour Guide Operators) kama ilivyo katika mikoa ya Kaskazini ambayo ina kampuni nyingi zinazofanya kazi za kitalii ambazo zimetoa ajira kwa vijana.
Utafiti umebaini kuwa katika mkoa wa Ruvuma,kuna maeneo mengine ya kihistoria hayawezi kufikika kwa sababu ya miundombinu mibovu na ufinyu wa bajeti inayotengwa kutembelea maeneo mengi yenye vivutio kwa mfano Njia ya Utumwa ya Kusini,Sultani Nampungu wa kabila la Wayao na Mapango ya Amanimakoro.
Challe anaitaja mikakati ambayo inachukuliwa kuboresha sekta ya utalii katika mkoa wa Ruvuma ni kulinda wanyamapori kwa kushirikina na wananchi,kuufanya Mji wa Mbambabay wilayani Nyasa kuwa mji wa kitalii,kushirikisha sekta binafsi kwenye utalii na kuvitangaza vivutio vya utalii kwa wananchi.
Mikakati mingine ni kutengeneza mtandao wa wa kiutalii Kanda ya Kusini na kwamba kwa kuwa mkoa wa Ruvuma una dalili ya kupata watalii toka Afrika ya Kusini ni vema Balozi Tanzania nchini Afrika Kusini,kusaidia kuongeza matangazo ya vivutio vya mkoa wa Ruvuma.
Mshauri huyo wa Maliasili na Utalii katika mkoa wa Ruvuma,anaomba mkoa uingizwe kwenye mradi wa kufungua utalii kanda ya kusini.Mpango huo utafanywa na serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Kwa ujumla mkoa wa Ruvuma bado una maliasili nyingi zikiwemo misitu,wanyamapori, samaki, mito, maziwa, milima, fukwe, mapango na rasilimali nyingine ambazo bado hazijaharibiwa hivyo zikiendelezwa zinaweza kutoa mchango mkubwa katika pato la Taifa na wananchi kupitia utalii.
Makala imeandikwa na Albano Midelo.ambaye ni Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.