MKOA WA RUVUMA WACHANGIA ASILIMIA 3.8 YA PATO LA TAIFA
UCHUMI wa Mkoa wa Ruvuma umeendelea kuimarika kwa kuchangia asilimia 3.8 ya pato la Taifa ukiwa juu ya mikoa mingine ya Kanda ya Kusini Mashariki.
Kwa mujibu wa Takwimu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu,uchumi wa Mkoa wa Ruvuma umeendelea kuimarika ambapo Pato la Taifa (GDP) kwa bei za mwaka husika,pato la Mkoa liliendelea kuongezeka kutoka shilingi bilioni 3.147 mwaka 2014 hadi kufikia shilingi bilioni 6.106 mwaka 2021.
Mchumi Mkuu kutoka Benki Kuu ya Tanzania(BOT) Kanda ya Mtwara Peter Stanlaus akizungumzia hali ya uchumi wa Mkoa wa Ruvuma kwenye kikao cha Baraza la Ushauri la Mkoa wa Ruvuma(RCC) amelitaja wastani la pato kwa mtu (GDP per capital) katika Mkoa limeendelea kuongezeka na kuwa juu ya wastani wa pato la mtu kitaifa.
“Wastani wa pato kwa mtu kwa mwaka katika Mkoa wa Ruvuma liliongezeka kutoka shilingi 2,184,532 mwaka 2014 hadi kufikia shilingi 3,602,162 mwaka 2021 ikilinganishwa na wastani wa pato kwa mtu kitaifa la shilingi 2,798,244 kwa mwaka’’,alisema.
Hata hivyo Mchumi Mkuu huyo wa BOT amesema hali ya mfumko wa bei katika Mkoa wa Ruvuma katika kipindi cha mwaka 2021/2022 ulibakia kwenye wastani wa asilimia 3.2 kutokana na kuimarika kwa ugavi wa chakula na kuongezeka kwa uzalishaji wa chakula.
Akizungumzia Mkoa wa Ruvuma ulivyochangia uchumi kupitia sekta ya madini,Mchumi Mkuu huyo wa BOT amesema sekta ya madini imeendelea kuimarika katika Kanda ya Kusini Mashariki ambapo kwa mwaka 2021/2022 ilichangia shilingi bilioni 728.9.
Hata hivyo ameutaja Mkoa wa Ruvuma kuwa katika sekta ya madini kwenye Kanda hiyo,ulichangia asilimia 69.9 ya thamani ya mapato yote ambapo uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe kutoka Ruvuma pekee umechangia asilimia 96.4 ya thamani ya madini yote kanda ya Kusini Mashariki.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo ya BOT,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amewapongeza wananchi wote wa Mkoa wa Ruvuma hasa kwenye sekta za kilimo na madini walivyoshiriki kikamilifu kuimarisha uchumi wa Mkoa.
“Kabla ya ripoti hii nilidhani naongoza Mkoa masikini,kumbe Mkoa wa Ruvuma ni Mkoa tajiri kwa sababu pato la mtu lipo juu ya wastani wa pato la mtu kitaifa’’.alisisitiza RC Thomas.
Mkoa wa Ruvuma umeendelea kuwa kapu la chakula la Taifa kwa kuongoza mfululizo kitaifa kwa miaka minne katika uzalishaji wa chakula nchini.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Desemba 31,2022
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.