MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Chritina Mndeme amewapongeza wakulima Mkoani Ruvuma kwa kuongoza mara mbili mfululizo kitaifa katika uzalishaji wa mazao ya chakula nchini.
Mndeme ametoa pongezi hizo wakati anafungua Kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Ruvuma kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea mjini Songea.
Akizungumzia muhtasari wa hali ya chakula na mavuno mkoani Ruvuma kwa mwaka 2019/2021.Mndeme amesema katika kioindi hicho mavuno yalikuwa ni tani 1,355,509 hali iliyoufanya Mkoa wa Ruvuma kuchukua nafasi ya kwanza kitaifa.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa amesema katika kipindi cha mwaka 2019/2021 mahitaji ya chakula katika Mkoa ni tani 469,172 hivyo Mkoa una ziada ya tani 886.337 na kwamba Mkoa umeendelea kufanya vizuri katika uzalishaji wa mazao ya Kilimo kwa mara ya pili mfululizo.
“Mafanikio haya ni matokeo ya wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kwa kuendelea kujituma katika shughuli za kilimo bila kulazimishwa na usimamizi mzuri wa maafisa ugani Ugani na viongozi wa Serikali”,alisema Mndeme.
Mdeme ameyataja mazao ya Ufuta,Mbaazi,na Soya kwa mwaka huu katika Mkoa Ruvuma yamefanyika kupitia mfumo wa stakabadhi ya Mazao ghalani hali ilisaidia kuingiza mapato ya zaidi ya shilingi bilioni 28.
Kati ya mapato hayo, Ufuta limeingiza zaidi ya shilingi bilioni 25,Soya zaidi ya shilingi bilioni moja na Mbaazi zaidi ya shilingi bilioni bili.
Mndeme amesema Mkoa unaendelea kushirikiana na Taasisi zingine za Serikali katika kusimamia zoezi la ununuzi wa Korosho kutoka kwa wakulima ambapo hadi sasa zimeuzwa kilo 14,826,644 zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 33.
Kwa mujibu wa Mndeme msimu wa Kilimo wa Mwaka 2020/2021 Mkoa umelenga kulima hekta 672,137 za mazao ya chakula na bustani na kuvuna tani 1,790,582 za mazao hayo.
Hata hivyo,amesema katika msimu wa mwaka 2020/2021 serikali itaendelea na mfumo wa bei elekezi wa kununua pembejeo za kilimo hususani Mbolea ya kupandia (DAP) na ya kukuzia (UREA),na Wizara ya Kilimo pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbolea Tanzania(TFRA)imetoa bei elekezi kwa kila Wilaya.
Mkoa wa Ruvuma ni gwiji katika uzalishaji wa chakula nchini baada ya kuongoza katika uzalishaji kitaifa kwa miaka miwili mfululizo.
Imeandaliwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Januari 13,2021
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.