Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma akabidhi gari la wagonjwa la kituo cha afya Mapera
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amekabidhi gari la kisasa la kubebea wagonjwa (Ambulance) la Kituo cha Afya Mapera Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga ambalo limenunuliwa kwa zaidi ya shilingi milioni 138.
Akitoa taarifa kabla ya uzinduzi na makabidhiano ya gari hilo kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma mjini Songea,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Juma Mnwele amesema wamefanikiwa kununua gari hilo kwa kutumia fedha za mapato ya ndani.
Amesema gari hilo la wagonjwa limekatiwa Bima kubwa (Premium) ya sh.milioni 6.3 na kwamba limepangiwa kutoa huduma za rufaa kwa wanawake,watoto na wagonjwa wengine katika kituo cha Afya Mapera ambacho kimejengwa kwa fedha za serikali kiasi cha shilingi milioni 400.
“Sisi watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga,tunaona fahari na faraja kuungana na Mhe.Rais John Magufuli ambaye alituletea milioni 400 za kujenga kituo cha afya Mapera na Halmashauri tumenunua gari la wagonjwa ,yawezekana haijawahi kufanyika mahala pengine’’,alisema Mnwele.
Akizungumza kabla ya uzinduzi na kukabidhi gari hilo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amewapongeza Halmashauri ya Mbinga kwa kuweza kununua gari la wagonjwa kwa kutumia fedha za mapato ya ndani.
Amesema Kituo cha afya Mapera ni kati ya vituo vya afya 16 vipya ambavyo vinajengwa katika Mkoa wa Ruvuma kutokana na fedha ambazo zimetolewa na Rais John Magufuli kwa lengo la kuboresha afya kwa wananchi wake.
Hata hivyo Mndeme amesema katika Halmashauri za Mkoa wa Ruvuma ujenzi wa hospitali nne za wilaya unaendelea kutekelezwa na kwamba serikali imedhamiria kuona Taifa na wananchi wanakuwa na afya bora ili waweze kutekeleza majukumu yao.
“Ninyi wananchi wa Mbinga kwa namna ya kipekee mmeamua kutumia fedha zenu za mapato ya ndani kununua ambulance ili kumuunga mkono Mhe.Rais wetu katika juhudi za kuboresha sekta ya afya kwa wananchi’’,alisisitiza.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ameziagiza Halmashauri nyingine mkoani humo kuiga mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga kutumia fedha za mapato ya ndani kununua ambulance kwa wale ambao hawana ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa magari ya wagonjwa.
Serikali imeajiri madaktari wapya 24 katika Mkoa wa Ruvuma ambao wamepangiwa kufanya kazi katika vituo vya afya na hospitali,ikiwemo madaktari wawili ambao wamepangiwa katika kituo cha afya Mapera.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Juni 16,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.