MKUU wa mkoa wa Ruvuma kanali Laban Thomas amesema,suala la upandaji miti katika wilaya zote tano za mkoa huo ni endelevu ili kusaidia kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji.
Laban ametoa agizo hilo kwenye uzinduzi wa zoezi la upandaji miti katika kijiji cha Kingerikiti kata ya Kingerikiti Halmashauri ya wilaya Nyasa,akiwa katika ziara ya kukagua miradi na shughuli mbalimbali za maendeleo wilayani humo.
Amewataka wananchi wa wilaya ya Nyasa,kuhakikisha wanaanzisha mashamba makubwa ya miti na anapanda angalau miti miwili kuzunguka maeneo yao kwani miti ni zao kubwa la biashara na lina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja,wilaya na mkoa wa Ruvuma.
Katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa ameeleza kuwa,serikali ya awamu ya sita kwa mwaka wa fedha 2021/2022 imetoa zaidi ya shilingi bilioni 10 kupitia fedha za mpango wa maendeleo na mapambano dhidi ya Uvico-19 kujenga vyumba vya madarasa katika wilaya zote za mkoa huo.
Aidha amesema,mkoa huo umepokea kiasi cha Shilingi bilioni 3.124 kwa ajili ya kujenga vyumba 110 vya madarasa ili kukabiliana na upunguzfu wa madarasa kwa shule za sekondari zilizopokea wanafunzi walioachaguliwa kuanza kidato cha kwanza kwa muhula wa masomo 2023.
Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa, mwaka 2022 mkoa wa Ruvuma umefanikiwa kujenga shule mpya za sekondari 11 katika Halmashauri zote nane za mkoa huo kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 7.7,vyumba 792 vya madarasa kwa shule za msingi na sekondari vyenye madawati,viti na meza.
Hata hivyo alisema,jambo la kusikitisha licha ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali lakini bado kuna wazazi hawajui umuhimu wa elimu kwa kutopeleka watoto wao shule.
“mheshimiwa Rais anaangaika kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga vyumba vya madarasa,lakini baadhi ya watu hawataki kupeleka watoto wao shule,sasa nawauliza mnataka wilaya yenu ya Nyasa kuwa na watu wa aina gani”alihoji Laban.
Alisema,serikali imejitahidi sana kutekeleza wajibu wake kwa kujenga vyumba vipya vya madarasa kila wilaya, kwa hiyo kilichobaki ni wazazi na jamii kuhakikisha watoto wao wanakwenda shule kupata elimu.
Edna Mahundi mkazi wa kijiji cha Kingerikiti,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi zilizowezesha kujengwa kwa vyumba na shule mpya za sekondari wilayani Nyasa.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.