Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abass Ahmed ametoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya Zaidi ya shilingi laki nane na fedha taslimu shilingi 690,000 kwa kituo cha Watoto yatima Chipole wilayani Songea.
Kituo hicho chenye Watoto yatima 74 kinamilikiwa na watawa wa Shirika la Mtakatifu Agnes Jimbo Kuu katoliki la Songea.
Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo,Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Abbas amevitaja vitu walivyopewa Watoto hao kuwa ni mchele kilo 100,maharage kilo 50,mafuta ya kupikia lita 20,sukari kilo 50,unga wa mahindi kilo 50 na sabuni ya unga mifuko miwili.
“Mimi binafsi nimekuwa na utamaduni katika maisha yangu,nikipata fursa huwa natembelea vituo vya kulelea Watoto yatima, kwa lengo la kuwashika mkono na kuwafariji huwa nafarijika ninapofanya jambo hili ’’,alisema RC Abbas.
Amewapongeza watawa hao kwa upendo mkubwa walionao kwa kuchukua jukumu la kuwahudumia Watoto yatima ambapo amesema jukumu hilo ni la kimungu Zaidi.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Rehema Madenge amewapongeza watawa hao kwa kwa kuwalea Watoto yatima 74 ambao amesema wanalelewa katika mikono salama kutokana na kituo hicho kuwa kimbilio la Watoto wengi.
Amesema kituo hicho kinaisaidia serikali kulea Watoto yatima na kwamba hakuna malipo yanayostahili kwa kazi hiyo Zaidi ya kuwaombea thawabu kwa mwenyezi Mungu.
Afisa Ustawi Mkoa wa Ruvuma Vikta Nyenza akitoa taarifa ya vituo vya kulelea yatima amesema katika Mkoa mzima kuna Watoto yatima 279 kati yao watoto 74 wanalelewa katika kituo cha Chipole.
Jumuiya ya watawa wa Chipole imemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kwa msaada wa vitu na fedha na kuwafariji na kuwatia moyo wa kuendelea kuwa na huruma na upendo wa kuwahudumia Watoto yatima.
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 S.L.P 74,SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.