SERIKALI mkoani Ruvuma imedhamiria kukuza sekta ya utalii na kuongeza idadi ya watalii wanaofika kutembelea vivutio lukuki vinavyopatikana ndani ya Mkoa.
Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Uchumi na Jamii(ESRF) Makao makuu jijini Dar es salaam Dr. Lunogelo Bohela akizungumza na wadau wa utalii mkoani Ruvuma ,amesema sekta hiyo kwa miaka mingi imekuwa inakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Kwa mujibu wa Bohela Taasisi yake inashirikiana na wataalam katika Mkoa wa Ruvuma ili kutengeneza mpango mkakati wa kuendeleza sekta ya utalii katika Mkoa wa Ruvuma.
“Sekta ya utalii nchini Tanzania ni ya muhimu sana kiuchumi,utalii unaposhamiri una faida kubwa kwa serikali na watu binafsi,utafiti unaonesha kuwa Mkoa wa Ruvuma kwa miaka mingi umekuwa nyuma kuvuna fursa za utalii’’,alisema Bohela.Kwa mujibu wa Mtafiti huyo Mwandamizi,katika watalii 300 wanaoingia Tanzania,Mkoa wa Ruvuma unapata mtalii mmoja tu jambo ambalo amesema limekuwa changamoto katika kukuza sekta ya utalii katika Mkoa huo.
Hata hivyo amesema Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa michache nchini yenye vivutio vya utalii vya aina mbalimbali na ambavyo havipatikani sehemu nyingine yeyote duniani .
Amevitaja miongoni mwa vivutio adimu katika Mkoa huo kuwa ni ziwa Nyasa ambalo ni kitovu cha utalii kutokana na kusheheni aina zote za vivutio vya utalii,vivutio vingine ni Hifadhi ya Taifa ya Nyerere,Makumbusho ya Taifa ya Majimaji,Mto Ruvuma,makanisa makongwe,ngoma za asili,utalii wa kilimo cha Ngoro,mapango na mawe ya kihistoria.
Ameutaja mpango mkakati wa kukuza sekta ya utalii katika Mkoa wa Ruvuma unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya serikali na Shirika la kimataifa la WWF unatarajia kusaidia kuinua pato linalotokana na utalii na kuchangia pato la Taifa na kwamba watalii wanapoingia kwa wingi wanasisimua shughuli za kiuchumi kutokana na kulala,kunywa na kusafiri.Akizungumza katika kikao hicho Katibu Tawala Msaidizi wa Huduma za Uchumi na Uzalishaji Jeremiah Sendoro amesema mpango mkakati huo utafanikiwa kwa sababu serikali imejitahidi kutatua changamoto zilizokuwa zinaikabili sekta ya utalii katika Mkoa wa Ruvuma.
Amesema serikali tayari imejenga miundombinu bora ya usafiri katika Mkoa wa Ruvuma zikiwemo barabara za lami,meli katika ziwa Nyasa,kuboresha uwanja wa ndege wa Songea, kuanzisha safari za ndege za abiria na wawekezaji kujenga hoteli za kisasa katika Mkoa wa Ruvuma.
Afisa Maliasili na Utalii wa Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe amesema ili mpango mkakati wa kukuza utalii upate matokeo chanya ni vema itolewe sera mpya ya utalii inayonufaisha mikoa ya kusini, elimu ya utalii iwe endelevu na matangazo ya kuvitangaza vivutio vya utalii mkoani Ruvuma yawe endelevu.
Imeandikwa na Albano Midelo
Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Oktoba 13,2020
Regional Commissioner Office
Anuwani: 1 TUNDURU ROAD, 57180 SONGEA, RUVUMA.
Simu: 0252602256
Simu ya Mkononi: 0252602256
Barua Pepe: ras.ruvuma@tamisemi.go.tz
Copyright ©2017 Ruvuma . All rights reserved.